Zaburi Mlango 22 Psalms

Zaburi 22:1

Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?

Zaburi 22:2

Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.

Zaburi 22:3

Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.

Zaburi 22:4

Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.

Zaburi 22:5

Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.

Zaburi 22:6

Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu.

Zaburi 22:7

Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;

Zaburi 22:8

Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.

Zaburi 22:9

Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.

Zaburi 22:10

Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.

Zaburi 22:11

Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.

Zaburi 22:12

Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga;

Zaburi 22:13

Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.

Zaburi 22:14

Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.

Zaburi 22:15

Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti

Zaburi 22:16

Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.

Zaburi 22:17

Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.

Zaburi 22:18

Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.

Zaburi 22:19

Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.

Zaburi 22:20

Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.

Zaburi 22:21

Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu.

Zaburi 22:22

Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.

Zaburi 22:23

Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.

Zaburi 22:24

Maana hakulidharau teso la mteswa, Wala hakuchukizwa nalo; Wala hakumficha uso wake, Bali alipomlilia akamsikia.

Zaburi 22:25

Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.

Zaburi 22:26

Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele.

Zaburi 22:27

Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia.

Zaburi 22:28

Maana ufalme una Bwana, Naye ndiye awatawalaye mataifa.

Zaburi 22:29

Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,

Zaburi 22:30

Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, Kwa kizazi kitakachokuja,

Zaburi 22:31

Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.