Zaburi Mlango 79 Psalms

Zaburi 79:1

Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako, Wamelinajisi hekalu lako takatifu. Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.

Zaburi 79:2

Wameziacha maiti za watumishi wako Ziwe chakula cha ndege wa angani. Na miili ya watauwa wako Iwe chakula cha wanyama wa nchi.

Zaburi 79:3

Wamemwaga damu yao kama maji Pande zote za Yerusalemu, Wala hapakuwa na mzishi.

Zaburi 79:4

Tumekuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

Zaburi 79:5

Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele? Wivu wako utawaka kama moto?

Zaburi 79:6

Ukali wako uwamwagie mataifa wasiokujua, Na falme za hao wasioliitia jina lako.

Zaburi 79:7

Kwa maana wamemla Yakobo, Na matuo yake wameyaharibu.

Zaburi 79:8

Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu, Rehema zako zije kutulaki hima, Kwa maana tumedhilika sana.

Zaburi 79:9

Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie, Kwa ajili ya utukufu wa jina lako. Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako.

Zaburi 79:10

Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Kisasi cha damu ya watumishi wako iliyomwagika Kijulike kati ya mataifa machoni petu.

Zaburi 79:11

Kuugua kwake aliyefungwa Na kuingie mbele zako. Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako Uwahifadhi wana wa mauti.

Zaburi 79:12

Uwalipe jirani zetu mara saba vifuani mwao Laumu zao walizokulaumu, Ee Bwana.

Zaburi 79:13

Na sisi tulio watu wako, Na kondoo za malisho yako, Tutakushukuru milele; Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.