Zaburi Mlango 40 Psalms

Zaburi 40:1

Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.

Zaburi 40:2

Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.

Zaburi 40:3

Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana

Zaburi 40:4

Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.

Zaburi 40:5

Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki.

Zaburi 40:6

Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.

Zaburi 40:7

Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)

Zaburi 40:8

Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.

Zaburi 40:9

Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.

Zaburi 40:10

Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa.

Zaburi 40:11

Nawe, Bwana, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.

Zaburi 40:12

Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha.

Zaburi 40:13

Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.

Zaburi 40:14

Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.

Zaburi 40:15

Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!

Zaburi 40:16

Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana.

Zaburi 40:17

Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.