Zaburi Mlango 148 Psalms

Zaburi 148:1

Haleluya. Msifuni Bwana kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu.

Zaburi 148:2

Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote.

Zaburi 148:3

Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga.

Zaburi 148:4

Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu.

Zaburi 148:5

Na vilisifu jina la Bwana, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.

Zaburi 148:6

Amevithibitisha hata milele na milele, Ametoa amri wala haitapita.

Zaburi 148:7

Msifuni Bwana kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote.

Zaburi 148:8

Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake.

Zaburi 148:9

Milima na vilima vyote, Miti yenye matunda na mierezi yote.

Zaburi 148:10

Hayawani, na wanyama wafugwao, Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa.

Zaburi 148:11

Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa dunia.

Zaburi 148:12

Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto;

Zaburi 148:13

Na walisifu jina la Bwana, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu.

Zaburi 148:14

Naye amewainulia watu wake pembe, Sifa za watauwa wake wote; Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. Haleluya.