Zaburi Mlango 80 Psalms

Zaburi 80:1

Wewe uchungaye Israeli, usikie, Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.

Zaburi 80:2

Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase, Uziamshe nguvu zako, Uje, utuokoe.

Zaburi 80:3

Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Zaburi 80:4

Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?

Zaburi 80:5

Umewalisha mkate wa machozi, Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.

Zaburi 80:6

Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.

Zaburi 80:7

Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Zaburi 80:8

Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.

Zaburi 80:9

Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.

Zaburi 80:10

Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.

Zaburi 80:11

Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.

Zaburi 80:12

Kwa nini umezibomoa kuta zake, Wakauchuma wote wapitao njiani?

Zaburi 80:13

Nguruwe wa msituni wanauharibu, Na hayawani wa kondeni wanautafuna.

Zaburi 80:14

Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.

Zaburi 80:15

Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.

Zaburi 80:16

Umechomwa moto; umekatwa; Kwa lawama ya uso wako wanapotea.

Zaburi 80:17

Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume; Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako;

Zaburi 80:18

Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma; Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.

Zaburi 80:19

Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.