Zaburi Mlango 85 Psalms

Zaburi 85:1

Bwana, umeiridhia nchi yako, Umewarejeza mateka wa Yakobo.

Zaburi 85:2

Umeusamehe uovu wa watu wako, Umezisitiri hatia zao zote.

Zaburi 85:3

Umeiondoa ghadhabu yako yote, Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.

Zaburi 85:4

Mungu wa wokovu wetu, uturudishe, Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.

Zaburi 85:5

Je! Utatufanyia hasira hata milele? Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi?

Zaburi 85:6

Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha, Watu wako wakufurahie?

Zaburi 85:7

Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Zaburi 85:8

Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena.

Zaburi 85:9

Hakika wokovu wake u karibu na wamchao, Utukufu ukae katika nchi yetu.

Zaburi 85:10

Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimehusiana.

Zaburi 85:11

Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni.

Zaburi 85:12

Naam, Bwana atatoa kilicho chema, Na nchi yetu itatoa mazao yake.

Zaburi 85:13

Haki itakwenda mbele zake, Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.