Zaburi Mlango 96 Psalms

Zaburi 96:1

Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Mwimbieni Bwana, nchi yote.

Zaburi 96:2

Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.

Zaburi 96:3

Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake.

Zaburi 96:4

Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.

Zaburi 96:5

Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.

Zaburi 96:6

Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.

Zaburi 96:7

Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu.

Zaburi 96:8

Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake.

Zaburi 96:9

Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.

Zaburi 96:10

Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki; Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike, Atawahukumu watu kwa adili.

Zaburi 96:11

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, Bahari na ivume na vyote viijazavyo,

Zaburi 96:12

Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;

Zaburi 96:13

Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake.