Zaburi Mlango 90 Psalms

Zaburi 90:1

Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi.

Zaburi 90:2

Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.

Zaburi 90:3

Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu.

Zaburi 90:4

Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.

Zaburi 90:5

Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo.

Zaburi 90:6

Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.

Zaburi 90:7

Maana tumetoweshwa kwa hasira yako, Na kwa ghadhabu yako tumefadhaishwa.

Zaburi 90:8

Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Siri zetu katika mwanga wa uso wako.

Zaburi 90:9

Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite.

Zaburi 90:10

Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.

Zaburi 90:11

Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako?

Zaburi 90:12

Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.

Zaburi 90:13

Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.

Zaburi 90:14

Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.

Zaburi 90:15

Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya.

Zaburi 90:16

Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao.

Zaburi 90:17

Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.