Zaburi Mlango 77 Psalms

Zaburi 77:1

Nimpazie Mungu sauti yangu, Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia.

Zaburi 77:2

Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika.

Zaburi 77:3

Nilipotaka kumkumbuka Mungu nalifadhaika; Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.

Zaburi 77:4

Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike; Naliona mashaka nisiweze kunena.

Zaburi 77:5

Nalifikiri habari za siku za kale, Miaka ya zamani zilizopita.

Zaburi 77:6

Nakumbuka wimbo wangu usiku, Nawaza moyoni mwangu, Roho yangu ikatafuta.

Zaburi 77:7

Je! Bwana atatupa milele na milele? Hatatenda fadhili tena kabisa?

Zaburi 77:8

Rehema zake zimekoma hata milele? Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote?

Zaburi 77:9

Mungu amesahau fadhili zake? Amezuia kwa hasira rehema zake?

Zaburi 77:10

Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo; Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kuume wake Aliye juu.

Zaburi 77:11

Nitayakumbuka matendo ya Bwana; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.

Zaburi 77:12

Pia nitaitafakari kazi yako yote; Nitaziwaza habari za matendo yako.

Zaburi 77:13

Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu?

Zaburi 77:14

Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.

Zaburi 77:15

Kwa mkono wako umewakomboa watu wako, Wana wa Yakobo na Yusufu.

Zaburi 77:16

Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka,

Zaburi 77:17

Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa.

Zaburi 77:18

Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika;

Zaburi 77:19

Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana.

Zaburi 77:20

Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni.