Zaburi Mlango 74 Psalms

Zaburi 74:1

Ee Mungu, mbona umetutupa milele? Kwa nini hasira yako inatoka moshi Juu ya kondoo wa malisho yako?

Zaburi 74:2

Ulikumbuke kusanyiko lako, Ulilolinunua zamani. Ulilolikomboa liwe kabila ya urithi wako, Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.

Zaburi 74:3

Upainulie miguu yako palipoharibika milele; Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.

Zaburi 74:4

Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako; Wameweka bendera zao ziwe alama.

Zaburi 74:5

Wanaonekana kama watu wainuao mashoka, Waikate miti ya msituni.

Zaburi 74:6

Na sasa nakishi yake yote pia Wanaivunja-vunja kwa mashoka na nyundo.

Zaburi 74:7

Wamepatia moto patakatifu pako; Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.

Zaburi 74:8

Walisema mioyoni mwao, Na tuwaangamize kabisa; Mahali penye mikutano ya Mungu Wamepachoma moto katika nchi pia.

Zaburi 74:9

Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii, Wala kwetu hakuna ajuaye, hata lini?

Zaburi 74:10

Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini? Adui alidharau jina lako hata milele?

Zaburi 74:11

Mbona unaurudisha mkono wako, Naam, mkono wako wa kuume, Uutoe kifuani mwako, Ukawaangamize kabisa.

Zaburi 74:12

Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani, Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi.

Zaburi 74:13

Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako, Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji.

Zaburi 74:14

Wewe uliviseta vichwa vya lewiathani, Awe chakula cha watu wa jangwani.

Zaburi 74:15

Wewe ulitokeza chemchemi na kijito; Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote.

Zaburi 74:16

Mchana ni wako, usiku nao ni wako, Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.

Zaburi 74:17

Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia, Kaskazi na kusi Wewe ulizitengeneza.

Zaburi 74:18

Ee Bwana, uyakumbuke hayo, adui amelaumu, Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako.

Zaburi 74:19

Usimpe mnyama mkali nafsi ya hua wako; Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.

Zaburi 74:20

Ulitafakari agano; Maana mahali penye giza katika nchi Pamejaa makao ya ukatili.

Zaburi 74:21

Aliyeonewa asirejee ametiwa haya, Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.

Zaburi 74:22

Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.

Zaburi 74:23

Usiisahau sauti ya watesi wako, Ghasia yao wanaokuondokea inapaa daima.