Zaburi Mlango 35 Psalms

Zaburi 35:1

Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.

Zaburi 35:2

Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.

Zaburi 35:3

Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako.

Zaburi 35:4

Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya.

Zaburi 35:5

Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.

Zaburi 35:6

Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia.

Zaburi 35:7

Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.

Zaburi 35:8

Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.

Zaburi 35:9

Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.

Zaburi 35:10

Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.

Zaburi 35:11

Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua.

Zaburi 35:12

Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa.

Zaburi 35:13

Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu.

Zaburi 35:14

Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye.

Zaburi 35:15

Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi.

Zaburi 35:16

Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno.

Zaburi 35:17

Bwana, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba.

Zaburi 35:18

Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.

Zaburi 35:19

Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e.

Zaburi 35:20

Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila.

Zaburi 35:21

Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona.

Zaburi 35:22

Wewe, Bwana, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami.

Zaburi 35:23

Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu.

Zaburi 35:24

Unihukumu kwa haki yako, Ee Bwana, Mungu wangu, Wala wasinisimangize.

Zaburi 35:25

Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza.

Zaburi 35:26

Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu.

Zaburi 35:27

Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake.

Zaburi 35:28

Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.