Zaburi Mlango 102 Psalms

Zaburi 102:1

Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.

Zaburi 102:2

Usinifiche uso wako siku ya shida yangu, Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.

Zaburi 102:3

Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga.

Zaburi 102:4

Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka, Naam, ninasahau kula chakula changu.

Zaburi 102:5

Kwa ajili ya sauti ya kuugua kwangu Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu.

Zaburi 102:6

Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani, Na kufanana na bundi wa mahameni.

Zaburi 102:7

Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro Aliye peke yake juu ya nyumba.

Zaburi 102:8

Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu Huapa kwa kunitaja mimi.

Zaburi 102:9

Maana nimekula majivu kama chakula, Na kukichanganya kinywaji changu na machozi.

Zaburi 102:10

Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako; Maana umeniinua na kunitupilia mbali.

Zaburi 102:11

Siku zangu zi kama kivuli kilichotandaa, Nami ninanyauka kama majani.

Zaburi 102:12

Bali Wewe, Bwana utaketi ukimiliki milele, Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.

Zaburi 102:13

Wewe mwenyewe utasimama, Na kuirehemu Sayuni, Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia, Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.

Zaburi 102:14

Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake, Na kuyaonea huruma mavumbi yake.

Zaburi 102:15

Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana, Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;

Zaburi 102:16

Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, Atakapoonekana katika utukufu wake,

Zaburi 102:17

Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao.

Zaburi 102:18

Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo, Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.

Zaburi 102:19

Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,

Zaburi 102:20

Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa.

Zaburi 102:21

Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni, Na sifa zake katika Yerusalemu,

Zaburi 102:22

Pindi mataifa watapokusanyika pamoja, Falme nazo ili kumtumikia Bwana.

Zaburi 102:23

Amezipunguza nguvu zangu njiani; Amezifupisha siku zangu.

Zaburi 102:24

Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.

Zaburi 102:25

Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako.

Zaburi 102:26

Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika.

Zaburi 102:27

Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma.

Zaburi 102:28

Wana wa watumishi wako watakaa, Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.