Zaburi Mlango 7 Psalms

Zaburi 7:1

Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.

Zaburi 7:2

Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.

Zaburi 7:3

Bwana, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya, Ikiwa mna uovu mikononi mwangu,

Zaburi 7:4

Ikiwa nimemlipa mabaya Yeye aliyekaa kwangu salama; (Hasha! Nimemponya yeye Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;)

Zaburi 7:5

Basi adui na anifuatie, Na kuikamata nafsi yangu; Naam, aukanyage uzima wangu, Na kuulaza utukufu wangu mavumbini.

Zaburi 7:6

Bwana uondoke kwa hasira yako; Ujiinue juu ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu.

Zaburi 7:7

Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale.

Zaburi 7:8

Bwana atawaamua mataifa, Bwana, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao.

Zaburi 7:9

Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki.

Zaburi 7:10

Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo.

Zaburi 7:11

Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.

Zaburi 7:12

Mtu asiporejea ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari;

Zaburi 7:13

Naye amemtengenezea silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto.

Zaburi 7:14

Tazama, huyu ana utungu wa uovu, Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo.

Zaburi 7:15

Amechimba shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya!

Zaburi 7:16

Madhara yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini.

Zaburi 7:17

Nitamshukuru Bwana kwa kadiri ya haki yake; Nitaliimbia jina la Bwana aliye juu.