Zaburi Mlango 45 Psalms

Zaburi 45:1

Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi.

Zaburi 45:2

Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.

Zaburi 45:3

Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako.

Zaburi 45:4

Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha.

Zaburi 45:5

Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme.

Zaburi 45:6

Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

Zaburi 45:7

Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako.

Zaburi 45:8

Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.

Zaburi 45:9

Binti za wafalme wamo Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki. Mkono wako wa kuume amesimama malkia Amevaa dhahabu ya Ofiri.

Zaburi 45:10

Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.

Zaburi 45:11

Naye mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.

Zaburi 45:12

Na binti Tiro analeta kipawa chake, Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako.

Zaburi 45:13

Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu, Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.

Zaburi 45:14

Atapelekwa kwa mfalme Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri. Wanawali wenzake wanaomfuata, Watapelekwa kwako.

Zaburi 45:15

Watapelekwa kwa furaha na shangwe, Na kuingia katika nyumba ya mfalme.

Zaburi 45:16

Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako, Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.

Zaburi 45:17

Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu Katika vizazi vyote. Kwa hiyo mataifa watakushukuru Milele na milele.