Zaburi Mlango 16 Psalms

Zaburi 16:1

Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.

Zaburi 16:2

Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako.

Zaburi 16:3

Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.

Zaburi 16:4

Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu.

Zaburi 16:5

Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu.

Zaburi 16:6

Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.

Zaburi 16:7

Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.

Zaburi 16:8

Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.

Zaburi 16:9

Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.

Zaburi 16:10

Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.

Zaburi 16:11

Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.