Ezekieli Mlango 7 Ezekiel

Ezekieli 7:1

Tena neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 7:2

Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU aiambia hivi nchi ya Israeli; Ni mwisho; mwisho umezijia pembe nne za nchi.

Ezekieli 7:3

Sasa mwisho huu unakupata, nami nitakuletea hasira yangu, nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.

Ezekieli 7:4

Jicho langu halitakuachilia, wala sitaona huruma; bali nitakupatiliza njia zako, na machukizo yako yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 7:5

Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, jambo baya la namna ya peke yake; angalia, linakuja.

Ezekieli 7:6

Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja.

Ezekieli 7:7

Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.

Ezekieli 7:8

Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.

Ezekieli 7:9

Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, napiga.

Ezekieli 7:10

Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka.

Ezekieli 7:11

Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao.

Ezekieli 7:12

Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata wote jamii.

Ezekieli 7:13

Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu wote jamii; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake.

Ezekieli 7:14

Wamepiga tarumbeta, wameweka vitu vyote tayari; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata wote jamii.

Ezekieli 7:15

Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla.

Ezekieli 7:16

Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake.

Ezekieli 7:17

Mikono yote itakuwa dhaifu, na magoti yote yatalegea kama maji.

Ezekieli 7:18

Tena watajifungia nguo za magunia, na utisho utawafunika; na aibu itakuwa juu ya nyuso zote, na upaa juu ya vichwa vyao vyote.

Ezekieli 7:19

Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya Bwana; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao.

Ezekieli 7:20

Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao.

Ezekieli 7:21

Nami nitapatia katika mikono ya wageni pawe mateka yao, na katika mikono ya waovu wa duniani pawe mawindo yao, nao watapanajisi.

Ezekieli 7:22

Tena nitaugeuza uso wangu usiwaelekee, nao watapatia unajisi mahali pangu pa siri; na wanyang'anyi wataingia humo na kupatia unajisi.

Ezekieli 7:23

Ufue mnyororo; kwa maana nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu.

Ezekieli 7:24

Kwa sababu hiyo nitawaleta watu wa mataifa walio wabaya kabisa, nao watazimiliki nyumba zao; tena nitakikomesha kiburi chao wenye nguvu; na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.

Ezekieli 7:25

Uharibifu unakuja; nao watatafuta amani, lakini haitapatikana.

Ezekieli 7:26

Madhara yatakuja juu ya madhara, na habari ya shari juu ya habari ya shari; nao watakwenda kwa nabii kutaka maono; lakini hiyo sheria itampotea kuhani, na mashauri yatawapotea wazee.

Ezekieli 7:27

Mfalme ataomboleza, na mkuu atavikwa ukiwa, na mikono ya watu wa nchi itataabika; nitawatenda sawasawa na njia yao; nami nitawahukumu sawasawa na kustahili kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.