Ezekieli Mlango 2 Ezekiel

Ezekieli 2:1

Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.

Ezekieli 2:2

Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.

Ezekieli 2:3

Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi; wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo.

Ezekieli 2:4

Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi.

Ezekieli 2:5

Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

Ezekieli 2:6

Na wewe, mwanadamu, usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na michongoma i pamoja nawe, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.

Ezekieli 2:7

Nawe utawaambia maneno yangu, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana.

Ezekieli 2:8

Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho.

Ezekieli 2:9

Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.

Ezekieli 2:10

Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!