Ezekieli Mlango 19 Ezekiel

Ezekieli 19:1

Tena uwaombolezee wakuu wa Israeli,

Ezekieli 19:2

useme, Mama yako alikuwa nini? Simba mke; alijilaza kati ya simba, kati ya wana-simba aliwalisha watoto wake.

Ezekieli 19:3

Akamlea mtoto mmoja katika watoto wake, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.

Ezekieli 19:4

Mataifa nao wakapata habari zake, akanaswa katika rima lao, wakamchukua kwa kulabu mpaka nchi ya Misri.

Ezekieli 19:5

Basi mamaye alipoona kwamba amemngoja, na tumaini lake limepotea, akatwaa mtoto mwingine katika watoto wake, akamfanya mwana-simba.

Ezekieli 19:6

Naye akaenda huko na huko kati ya simba, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.

Ezekieli 19:7

Akayajua majumba yao, akaiharibu miji yao; nchi ikawa ukiwa, navyo vitu vilivyoijaza, kwa sababu ya mshindo wa kunguruma kwake.

Ezekieli 19:8

Ndipo mataifa wakajipanga juu yake pande zote toka nchi zote; wakaunda wavu wao juu yake; akanaswa katika rima lao.

Ezekieli 19:9

Wakamtia katika tundu kwa kulabu, wakamleta kwa mfalme wa Babeli wakamtia ndani ya ngome, sauti yake isisikiwe tena juu ya milima ya Israeli.

Ezekieli 19:10

Mama yako alikuwa kama mzabibu, katika damu yako, uliopandwa karibu na maji; akazaa sana na kujaa matawi, kwa sababu ya maji mengi.

Ezekieli 19:11

Naye alikuwa na vijiti vya nguvu, kwa fimbo za enzi zao watawalao, na kimo chao kiliinuka kati ya matawi manene, wakaonekana kwa urefu wao, pamoja na wingi wa matawi yao.

Ezekieli 19:12

Lakini aling'olewa kwa ghadhabu, akaangushwa chini, upepo wa mashariki ukakausha matunda yake; vijiti vyake vya nguvu vikavunjika, vikakauka; moto ulivila.

Ezekieli 19:13

Na sasa umepandwa jangwani, katika nchi kavu, ya ukame.

Ezekieli 19:14

Na moto umetoka katika vijiti vya matawi yake, umekula matunda yake, hata hana tena kijiti cha nguvu kifaacho kwa fimbo ya enzi ya kutawala. Na hayo ni maombolezo, nayo yatakuwa maombolezo.