Ezekieli Mlango 10 Ezekiel

Ezekieli 10:1

Ndipo nikaangalia, na tazama, katika anga lililokuwa juu ya vichwa vya makerubi, kulionekana juu yao kana kwamba ni yakuti samawi, kuonekana kama mfano wa kiti cha enzi.

Ezekieli 10:2

Naye akamwambia mtu yule aliyevaa bafta, akasema, Ingia kati ya magurudumu yazungukayo, yaani, chini ya kerubi, ukaijaze mikono yako yote miwili makaa ya moto, toka katikati ya makerubi, ukayamwage juu ya mji. Akaingia ndani mbele ya macho yangu.

Ezekieli 10:3

Basi, makerubi walisimama upande wa kuume wa nyumba, hapo alipoingia mtu yule; nalo wingu likaujaza ua wa ndani.

Ezekieli 10:4

Utukufu wa Bwana ukapaa kutoka kwa kerubi yule, ukasimama juu ya kizingiti cha nyumba; nayo nyumba ikajazwa na lile wingu, na ua ulikuwa umejaa mwangaza wa utukufu wa Bwana.

Ezekieli 10:5

Na sauti ya mabawa ya makerubi ikasikiwa, hata katika ua wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi, asemapo.

Ezekieli 10:6

Ikawa, hapo alipomwagiza huyo mtu aliyevaa bafta, akisema, Twaa moto kutoka katikati ya magurudumu yazungukayo katikati ya hao makerubi, akaingia, akasimama karibu na gurudumu moja.

Ezekieli 10:7

Na kerubi yule akanyosha mkono wake toka katikati ya makerubi, kwa moto ule uliokuwa katikati ya makerubi, akatwaa baadhi ya moto ule, akautia katika mikono ya mtu yule aliyevaa bafta; naye akautwaa, akatoka.

Ezekieli 10:8

Kukaonekana katika makerubi mfano wa mkono wa mwanadamu chini ya mabawa yao.

Ezekieli 10:9

Nami nikaangalia, na tazama, yalikuwako magurudumu manne karibu na makerubi, gurudumu moja karibu na kerubi mmoja, na gurudumu lingine karibu na kerubi mwingine; na kuonekana kwa magurudumu kulikuwa kana kwamba ni zabarajadi.

Ezekieli 10:10

Na kuonekana kwake, yote manne yalikuwa na mfano mmoja, kana kwamba gurudumu moja lilikuwa ndani ya gurudumu lingine.

Ezekieli 10:11

Walipokwenda, walikwenda kwa pande zao nne; hawakugeuka walipokwenda, lakini walifuata mpaka mahali pale kilipopaelekea kichwa; hawakugeuka walipokwenda.

Ezekieli 10:12

Na mwili wao mzima, na maungo yao, na mikono yao, na mabawa yao, na magurudumu, wamejaa macho pande zote, hata magurudumu waliyokuwa nayo wale wanne.

Ezekieli 10:13

Na magurudumu hayo yaliitwa Kisulisuli, nami nalisikia.

Ezekieli 10:14

Kila mmoja alikuwa na nyuso nne; uso wa kwanza ulikuwa uso wa kerubi, na uso wa pili ulikuwa uso wa mwanadamu, na uso wa tatu ulikuwa uso wa simba, na uso wa nne ulikuwa uso wa tai.

Ezekieli 10:15

Makerubi wakapaa juu; huyo ndiye kiumbe hai niliyemwona karibu na mto Kebari.

Ezekieli 10:16

Na makerubi walipokwenda, magurudumu yale yalikwenda kando yao; na makerubi walipoinua mabawa yao, wapate kupaa juu kutoka katika dunia, magurudumu yale hayakugeuka wala kutoka kando yao.

Ezekieli 10:17

Waliposimama hao, hayo nayo yalisimama; na walipopaa juu hao, hayo nayo yalipaa juu pamoja nao; maana roho ya huyo kiumbe hai ilikuwa ndani yao.

Ezekieli 10:18

Kisha huo utukufu wa Bwana ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi.

Ezekieli 10:19

Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.

Ezekieli 10:20

Huyu ndiye kiumbe hai niliyemwona, chini ya Mungu wa Israeli, karibu na mto Kebari; nikajua ya kuwa hao ni makerubi.

Ezekieli 10:21

Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne; na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao.

Ezekieli 10:22

Na mfano wa nyuso zao, ni nyuso zile zile nilizoziona karibu na mto Kebari; kuonekana kwao, na wao wenyewe; kila mmoja walikwenda mbele moja kwa moja.