Ezekieli Mlango 20 Ezekiel

Ezekieli 20:1

Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa Bwana, wakaketi mbele yangu.

Ezekieli 20:2

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 20:3

Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi.

Ezekieli 20:4

Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao;

Ezekieli 20:5

uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni Bwana, Mungu wenu;

Ezekieli 20:6

katika siku ile naliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;

Ezekieli 20:7

nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni Bwana, Mungu wenu.

Ezekieli 20:8

Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri.

Ezekieli 20:9

Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nalijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri.

Ezekieli 20:10

Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani.

Ezekieli 20:11

Nikawapa amri zangu, na kuwaonyesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda.

Ezekieli 20:12

Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.

Ezekieli 20:13

Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize.

Ezekieli 20:14

Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao naliwatoa mbele ya macho yao.

Ezekieli 20:15

Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;

Ezekieli 20:16

kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao.

Ezekieli 20:17

Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.

Ezekieli 20:18

Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao.

Ezekieli 20:19

Mimi ni Bwana, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda;

Ezekieli 20:20

zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Ezekieli 20:21

Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.

Ezekieli 20:22

Lakini naliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao naliwatoa.

Ezekieli 20:23

Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali;

Ezekieli 20:24

kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao.

Ezekieli 20:25

Tena naliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo;

Ezekieli 20:26

nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 20:27

Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wamekosa kosa juu yangu.

Ezekieli 20:28

Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifanya nukato la kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa.

Ezekieli 20:29

Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo.

Ezekieli 20:30

Basi, uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mnajitia unajisi kwa kuzifuata njia za baba zenu? Mnakwenda kufanya uasherati kwa kuyafuata machukizo yao?

Ezekieli 20:31

Tena mtoapo matoleo yenu, na kuwapitisha watoto wenu motoni, je! Mnajitia unajisi kwa vinyago vyenu vyote hata leo? Na mimi je! Niulizwe neno nanyi, Enyi nyumba ya Israeli? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi.

Ezekieli 20:32

Na haya yote yaingiayo katika nia zenu hayatakuwa kamwe; ikiwa mmesema, Sisi tutakuwa sawasawa na mataifa, sawasawa na jamaa za nchi nyingine, kutumikia miti na mawe.

Ezekieli 20:33

Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu;

Ezekieli 20:34

nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika;

Ezekieli 20:35

nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso.

Ezekieli 20:36

Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 20:37

Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano.

Ezekieli 20:38

Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 20:39

Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Enendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu.

Ezekieli 20:40

Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote.

Ezekieli 20:41

Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa.

Ezekieli 20:42

Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu.

Ezekieli 20:43

Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda.

Ezekieli 20:44

Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si sawasawa na njia zenu mbaya, wala si sawasawa na matendo yenu mabovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 20:45

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 20:46

Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu,

Ezekieli 20:47

ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la Bwana; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hata kaskazini zitateketezwa kwa moto huo.

Ezekieli 20:48

Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, Bwana, nimeuwasha; hautazimika.

Ezekieli 20:49

Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, wao hunisema; Je! Mtu huyu si mtu mwenye kupiga mithali?