Ezekieli Mlango 12 Ezekiel

Ezekieli 12:1

Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

Ezekieli 12:2

Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi.

Ezekieli 12:3

Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi.

Ezekieli 12:4

Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watokavyo katika kuhamishwa.

Ezekieli 12:5

Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale.

Ezekieli 12:6

Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi; kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli.

Ezekieli 12:7

Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nalitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao.

Ezekieli 12:8

Asubuhi neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 12:9

Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, Unafanya nini wewe?

Ezekieli 12:10

Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao.

Ezekieli 12:11

Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa.

Ezekieli 12:12

Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake.

Ezekieli 12:13

Tena wavu wangu nitautandika juu yake, naye atanaswa kwa mtego wangu; nami nitampeleka Babeli, mpaka nchi ya Wakaldayo; lakini hataiona, angawa atakufa huko.

Ezekieli 12:14

Nami nitawatawanya kwa pepo zote wote wamzungukao ili wamsaidie, na vikosi vyake vyote; nami nitaufuta upanga nyuma yao.

Ezekieli 12:15

Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatupa-tupa katika nchi zote.

Ezekieli 12:16

Lakini nitawasaza watu wachache miongoni mwao na kuwaokoa na upanga, na njaa, na tauni ili watangaze habari ya machukizo yao yote, kati ya mataifa huko waendako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 12:17

Tena neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 12:18

Mwanadamu, ule chakula chako kwa matetemo, ukanywe maji yako kwa kutetemeka na kwa kuyatunza sana;

Ezekieli 12:19

ukawaambie watu wa nchi, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari zao wakaao Yerusalemu, na katika nchi ya Israeli; Watakula chakula chao kwa kukitunza sana, na maji yao watayanywa kwa ushangao, nchi yao iwe ukiwa, kwa kukosa vitu vyote viijazavyo, kwa sababu ya udhalimu wao wote wakaao ndani yake.

Ezekieli 12:20

Na miji yote yenye watu itakuwa maganjo, nayo nchi itakuwa ukiwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 12:21

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 12:22

Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi.

Ezekieli 12:23

Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote.

Ezekieli 12:24

Kwa maana hayatakuwapo tena maono yo yote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli.

Ezekieli 12:25

Maana mimi ni Bwana; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 12:26

Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

Ezekieli 12:27

Mwanadamu, tazama, hao wa nyumba ya Israeli husema, Maono hayo ayaonayo ni ya siku nyingi zijazo, naye anatabiri habari ya nyakati zilizo mbali sana.

Ezekieli 12:28

Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Maneno yangu hayatakawilishwa tena hata moja, bali neno nitakalolinena litatimizwa, asema Bwana MUNGU.