Ezekieli Mlango 3 Ezekiel

Ezekieli 3:1

Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.

Ezekieli 3:2

Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.

Ezekieli 3:3

Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.

Ezekieli 3:4

Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.

Ezekieli 3:5

Maana wewe hukutumwa kwa watu wa maneno mageni, ama wa lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli;

Ezekieli 3:6

si kwa watu wa kabila nyingi wenye maneno mageni, na lugha ngumu, ambao huwezi kufahamu maneno yao. Bila shaka, kama ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.

Ezekieli 3:7

Bali nyumba ya Israeli hawatakusikiliza wewe; kwa kuwa hawanisikilizi mimi; maana nyumba yote ya Israeli wana vipaji vigumu, na mioyo yenye ukaidi.

Ezekieli 3:8

Tazama, nimeufanya uso wako kuwa mgumu juu ya nyuso zao, na kipaji cha uso chako kuwa kigumu juu ya vipaji vya nyuso vyao.

Ezekieli 3:9

Kama almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji chako; usiwaogope, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.

Ezekieli 3:10

Tena akaniambia, Mwanadamu, maneno yangu yote nitakayokuambia, yapokee moyoni mwako, na kuyasikia kwa masikio yako.

Ezekieli 3:11

Haya! Enenda uwafikilie watu hao waliohamishwa, kwa wana wa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, Bwana MUNGU asema hivi; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia.

Ezekieli 3:12

Ndipo roho ikaniinua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama mshindo wa radi kuu, ikisema, Na uhimidiwe utukufu wa Bwana tokea mahali pake.

Ezekieli 3:13

Nikasikia mshindo wa mabawa ya vile viumbe hai, walipogusana, na mshindo wa yale magurudumu kando yao, mshindo wa radi kuu.

Ezekieli 3:14

Basi roho ikaniinua, ikanichukua mahali pengine; nami nikaenda kwa uchungu, na hasira kali rohoni mwangu, na mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu kwa nguvu.

Ezekieli 3:15

Ndipo nikawafikia watu waliohamishwa, huko Tel-abibu, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari, nikafika huko walikokuwa wakikaa; nikaketi huko miongoni mwao muda wa siku saba, katika hali ya ushangao mwingi.

Ezekieli 3:16

Hata ikawa, mwisho wa siku saba, neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 3:17

Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.

Ezekieli 3:18

Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.

Ezekieli 3:19

Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.

Ezekieli 3:20

Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.

Ezekieli 3:21

Bali ukimwonya mwenye haki, kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikiwa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa; nawe umejiokoa roho yako.

Ezekieli 3:22

Na mkono wa Bwana ulikuwako juu yangu huko; akaniambia, Ondoka, enenda uwandani; nami nitasema nawe huko.

Ezekieli 3:23

Basi, nikaondoka, nikaenda uwandani, na tazama, utukufu wa Bwana ulisimama huko, kama utukufu ule niliouona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.

Ezekieli 3:24

Ndipo roho ile ikaniingia, ikanisimamisha kwa miguu yangu; akasema nami, akaniambia, Enenda ukajifungie nyumbani mwako.

Ezekieli 3:25

Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu, nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao;

Ezekieli 3:26

nami nitaufanya ulimi wako ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao; kwa kuwa wao ni nyumba yenye kuasi.

Ezekieli 3:27

Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua kinywa chako, nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Yeye asikiaye na asikie; naye akataaye na akatae; maana wao ni nyumba yenye kuasi.