Ezekieli Mlango 21 Ezekiel

Ezekieli 21:1

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 21:2

Mwanadamu, uelekeze uso wako kuelekea Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli;

Ezekieli 21:3

uiambie nchi ya Israeli, Bwana asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya.

Ezekieli 21:4

Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hata kaskazini,

Ezekieli 21:5

na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena.

Ezekieli 21:6

Ugua, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika kwake viuno vyako, na kwa uchungu, utaugua mbele ya macho yao.

Ezekieli 21:7

Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unaugua? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatalegea kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 21:8

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 21:9

Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa,

Ezekieli 21:10

umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti.

Ezekieli 21:11

Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye.

Ezekieli 21:12

Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani.

Ezekieli 21:13

Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 21:14

Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote.

Ezekieli 21:15

Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje.

Ezekieli 21:16

Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako.

Ezekieli 21:17

Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, Bwana, nimenena neno hili.

Ezekieli 21:18

Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

Ezekieli 21:19

Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini.

Ezekieli 21:20

Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma.

Ezekieli 21:21

Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini.

Ezekieli 21:22

Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome.

Ezekieli 21:23

Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe.

Ezekieli 21:24

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono.

Ezekieli 21:25

Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho;

Ezekieli 21:26

Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka.

Ezekieli 21:27

Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa.

Ezekieli 21:28

Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari za wana wa Amoni, na katika habari za aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umesuguliwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme;

Ezekieli 21:29

wakati wakuoneapo ubatili, wakati wakufanyiao uganga wa uongo, ili kukuweka juu ya shingo zao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho.

Ezekieli 21:30

Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe.

Ezekieli 21:31

Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza.

Ezekieli 21:32

Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itakuwa katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, Bwana, nimenena neno hili.