Ezekieli Mlango 25 Ezekiel

Ezekieli 25:1

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 25:2

Mwanadamu, uwaelekezee wana wa Amoni uso wako, ukatabiri juu yao.

Ezekieli 25:3

Uwaambie hao wana wa Amoni, Lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umesema, Aha! Juu ya patakatifu pangu, palipotiwa unajisi; na juu ya nchi ya Israeli, ilipoharibiwa; na juu ya nyumba ya Israeli, walipokwenda kifungoni;

Ezekieli 25:4

basi, kwa sababu hiyo, nitakutia katika mikono ya wana wa mashariki uwe milki yao, nao wataweka marago yao ndani yako, kufanya maskani zao ndani yako; watakula matunda yako, na kunywa maziwa yako.

Ezekieli 25:5

Nami nitafanya Raba kuwa banda la ngamia, na wana wa Amoni kuwa mahali pa kulaza makundi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 25:6

Maana Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umepiga makofi, na kupiga mshindo kwa miguu yako, na kufurahi juu ya nchi ya Israeli, jeuri yote ya roho yako;

Ezekieli 25:7

basi, tazama, nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nitakutoa uwe mateka ya mataifa; nami nitakukatilia mbali na kabila za watu, nami nitakuangamiza, usiwe katika nchi hizo; nitakukomesha; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 25:8

Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu Moabu na Seiri husema, Tazama, nyumba ya Israeli ni sawasawa na mataifa yote;

Ezekieli 25:9

basi, tazama, nitawafunulia wana wa mashariki ubavu wa Moabu toka miji yake, toka miji yake iliyo mipakani mwake, utukufu wa nchi hiyo, Beth-yeshimothi, na Baal-meoni, na Kiriathaimu,

Ezekieli 25:10

pamoja na wana wa Amoni, nami nitawatoa kuwa milki, ili wana wa Amoni wasikumbukwe kati ya mataifa,

Ezekieli 25:11

nami nitatoa hukumu juu ya Moabu; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 25:12

Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Edomu wametenda kinyume cha nyumba ya Yuda, kwa kujilipiza kisasi, nao wamekosa sana, na kujilipiza kisasi juu yao;

Ezekieli 25:13

kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Nitanyosha mkono wangu juu ya Edomu, nitakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama; nami nitaifanya kuwa ukiwa toka Temani; na mpaka Dedani wataanguka kwa upanga.

Ezekieli 25:14

Nami nitaweka kisasi changu juu ya Edomu, kwa mkono wa watu wangu Israeli; nao watatenda mambo katika Edomu, kwa kadiri ya hasira yangu, na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 25:15

Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Wafilisti wametenda mambo kwa kujilipiza kisasi, nao wamejilipiza kisasi kwa jeuri ya roho, ili kupaangamiza kwa uadui wa daima;

Ezekieli 25:16

kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitanyosha mkono wangu juu ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi, na kuwaharibu wabakio pande za pwani.

Ezekieli 25:17

Nami nitajilipiza kisasi kikuu, nikiwakemea kwa ukali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapojilipiza kisasi juu yao.