Ezekieli Mlango 17 Ezekiel

Ezekieli 17:1

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 17:2

Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali;

Ezekieli 17:3

useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi;

Ezekieli 17:4

akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi.

Ezekieli 17:5

Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto.

Ezekieli 17:6

Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko.

Ezekieli 17:7

Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha.

Ezekieli 17:8

Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri.

Ezekieli 17:9

Basi nena wewe, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Huo utafanikiwa? Yeye hataing'oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ili ukauke? Kwamba majani mabichi yake yote yachipukayo yakauke, hata ikiwa hana nguvu nyingi, wala watu wengi wa kuung'oa na mizizi yake?

Ezekieli 17:10

Naam, tazama, ingawa umepandwa, je! Utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo wa mashariki utakapoupiga? Naam, utakauka katika matuta hapo ulipopandwa.

Ezekieli 17:11

Tena neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 17:12

Waambie sasa nyumba hii iliyoasi, Hamjui maana ya mambo haya? Waambie, Tazama, mfalme wa Babeli alifika Yerusalemu, akamtwaa mfalme wake, na wakuu wake, akawachukua pamoja naye mpaka Babeli;

Ezekieli 17:13

akawatwaa baadhi ya wazao wa kifalme; kisha akafanya agano naye, akamwapisha; akawaondoa watu wa nchi wenye nguvu;

Ezekieli 17:14

ili ufalme huo uwe duni usijiinue, lakini usimame kwa kulishika agano lake.

Ezekieli 17:15

Lakini alimwasi kwa kupeleka wajumbe huko Misri, wampe farasi na watu wengi. Je! Atafanikiwa? Afanyaye mambo hayo ataokoka? Atalivunja agano, kisha akaokoka?

Ezekieli 17:16

Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika mahali pale akaapo mfalme aliyemmilikisha, ambaye alikidharau kiapo chake, na kulivunja agano lake, ndipo atakapokufa pamoja naye kati ya Babeli.

Ezekieli 17:17

Wala Farao na jeshi lake kubwa, na kusanyiko lake kuu la watu, hawatamfaa kitu vitani, watakapofanya maboma, na kujenga ngome, ili kukatilia mbali watu wengi.

Ezekieli 17:18

Kwa maana amekidharau kiapo kwa kulivunja agano; na tazama, ametia mkono wake, na pamoja na hayo ameyatenda mambo hayo yote; hataokoka.

Ezekieli 17:19

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika kiapo changu alichokidharau, na agano langu alilolivunja, nitampatiliza kichwani pake.

Ezekieli 17:20

Nami nitatandika wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu, nami nitamleta hata Babeli; nami nitateta naye huko kwa sababu ya kosa lake alilonikosa.

Ezekieli 17:21

Na wakimbizi wake wote wa vikosi vyake vyote wataanguka kwa upanga, na hao watakaosalia watatawanyika kwenye kila upepo; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimenena neno hili.

Ezekieli 17:22

Bwana MUNGU asema hivi; Mimi nami nitakitwaa kilele kirefu cha mwerezi, na kukipandikiza mahali; na katika vitawi vyake vilivyo juu nitatwaa kitawi kimoja kilicho chororo, nami nitakipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana;

Ezekieli 17:23

juu ya mlima wa mahali palipoinuka pa Israeli nitakipanda; nacho kitatoa matawi, na kuzaa matunda, nao utakuwa mwerezi mzuri; na chini yake watakaa ndege wa kila namna ya mbawa; katika uvuli wa matawi yake watakaa.

Ezekieli 17:24

Na miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu, na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuusitawisha mti mkavu; mimi, Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili.