Ezekieli Mlango 13 Ezekiel

Ezekieli 13:1

Kisha neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 13:2

Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la Bwana;

Ezekieli 13:3

Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!

Ezekieli 13:4

Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.

Ezekieli 13:5

Hamkupanda kwenda mahali palipobomolewa, wala hamkuitengenezea nyumba ya Israeli boma, wapate kusimama vitani katika siku ya Bwana.

Ezekieli 13:6

Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, Bwana asema; lakini Bwana hakuwatuma; nao wamewatumainisha watu ya kuwa neno lile litatimizwa.

Ezekieli 13:7

Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena mabashiri ya uongo? Nanyi mwasema, Bwana asema; ila mimi sikusema neno.

Ezekieli 13:8

Basi tazama, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu mmenena ubatili, na kuona uongo, basi, kwa sababu hiyo, mimi ni juu yenu, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 13:9

Na mkono wangu utakuwa juu ya manabii wanaoona ubatili, na kutabiri uongo; hawatakuwa katika mashauri ya watu wangu, wala hawataandikwa katika maandiko ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

Ezekieli 13:10

Kwa sababu hiyo, kwa sababu wameshawishi watu wangu, wakisema, Amani; wala hapana amani; na mtu mmoja ajengapo ukuta, tazama, waupaka chokaa isiyokorogwa vema;

Ezekieli 13:11

basi waambie hao wanaoupaka ukuta chokaa isiyokorogwa vema, ya kwamba utaanguka; kutakuwa mvua ya kufurika; nanyi, enyi mvua ya mawe makubwa ya barafu, mtaanguka; na upepo wa dhoruba utaupasua.

Ezekieli 13:12

Na huo ukuta utakapoanguka, je! Hamtaambiwa, Ku wapi kupaka kwenu mlikoupaka?

Ezekieli 13:13

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Nitaupasua kwa upepo wa dhoruba, katika ghadhabu yangu; tena kutakuwa mvua ya barafu ya kufurika katika hasira yangu; na mawe makubwa ya barafu katika hasira ya kuukomesha.

Ezekieli 13:14

Ndivyo nitakavyoubomoa ukuta mlioupaka chokaa isiyokorogwa vema, na kuuangusha chini, hata misingi yake itafunuliwa; nao utaanguka, nanyi mtaangamizwa katikati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 13:15

Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu juu ya ukuta ule, na juu yao walioupaka chokaa isiyokorogwa vema; nami nitawaambieni, Ukuta huo hauko sasa, wala wao walioupaka hawako;

Ezekieli 13:16

yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 13:17

Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao,

Ezekieli 13:18

useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe?

Ezekieli 13:19

Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo.

Ezekieli 13:20

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege.

Ezekieli 13:21

Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 13:22

Kwa kuwa ninyi mmemhuzunisha moyo mwenye haki kwa uongo, ambaye mimi sikumhuzunisha; na kuitia nguvu mikono ya mtu mbaya, hata asigeuke, na kuiacha njia yake mbaya, na kuhifadhika;

Ezekieli 13:23

basi, kwa sababu hiyo ninyi hamtaona tena ubatili, wala kutabiri mambo; nami nitawaokoa watu wangu katika mikono yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.