Ezekieli Mlango 24 Ezekiel

Ezekieli 24:1

Tena, katika mwaka wa kenda, mwezi wa kumi, siku ya kumi ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 24:2

Mwanadamu, liandike jina la siku hii, naam, la siku ii hii; mfalme wa Babeli ameukaribia Yerusalemu siku iyo hiyo.

Ezekieli 24:3

Ukawatungie mithali nyumba ya kuasi, ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Teleka sufuria, liteleke; ukatie maji ndani yake;

Ezekieli 24:4

vikusanye vipande vyake ndani yake, naam, kila kipande chema, paja na bega; lijaze mifupa iliyochaguliwa.

Ezekieli 24:5

Uwatwae wateule wa kundi la kondoo, ukafanye chungu ya mifupa chini yake; ukalitokose sana; naam, mifupa yake itokoswe ndani yake.

Ezekieli 24:6

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Hilo sufuria ambalo kutu yake i ndani yake, ambalo kutu yake haikulitoka; litoe kipande kipande; hapana kura iliyoanguka juu yake.

Ezekieli 24:7

Maana damu yake imo ndani yake; aliiweka juu ya jabali lililo wazi; hakuimwaga juu ya nchi, apate kuifunika kwa mavumbi;

Ezekieli 24:8

ili ipandishe ghadhabu ya kulipa kisasi, nimeiweka damu yake juu ya jabali lililo wazi, isipate kufunikwa.

Ezekieli 24:9

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Mimi nami nitaiongeza chungu.

Ezekieli 24:10

Tia kuni nyingi, uchochee moto, itokose nyama sana, fanyiza mchuzi mzito, mifupa ikateketee.

Ezekieli 24:11

Kisha litie juu ya makaa yake, tupu, lipate moto, na shaba yake iteketee, uchafu wake uyeyushwe, na kutu yake iteketee.

Ezekieli 24:12

Amejidhoofisha kwa taabu, lakini kutu yake nyingi haikumtoka; kutu yake haitoki kwa moto.

Ezekieli 24:13

Katika uchafu wako mna uasherati, kwa maana nimekusafisha, ila wewe hukusafika; hutasafishwa tena uchafu wako ukutoke, hata nitakapokuwa nimeituliza hasira yangu kwako.

Ezekieli 24:14

Mimi, Bwana, nimenena neno hili, nalo litakuwa; nami nitalifanya; sitaachilia, wala sitahurumia, wala sitajuta; sawasawa na njia zako, na sawasawa na matendo yako, ndivyo watakavyokuhukumu, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 24:15

Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

Ezekieli 24:16

Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako.

Ezekieli 24:17

Ugua lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu.

Ezekieli 24:18

Basi nalisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami nalifanya asubuhi kama nilivyoagizwa.

Ezekieli 24:19

Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo.

Ezekieli 24:20

Nikawaambia, Neno la Bwana lilinijia, kusema,

Ezekieli 24:21

Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga.

Ezekieli 24:22

Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu.

Ezekieli 24:23

Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kuugua kila mtu pamoja na mwenziwe.

Ezekieli 24:24

Basi ndivyo Ezekielii atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

Ezekieli 24:25

Nawe, mwanadamu, je! Haitakuwa hivi katika siku hiyo nitakapowaondolea nguvu zao, na furaha ya utukufu wao, na kilichotamaniwa na macho yao, ambacho walikiinulia mioyo yao, wana wao na binti zao,

Ezekieli 24:26

kwamba katika siku iyo hiyo yeye atakayeokoka atakuja kwako, akusikize jambo hili kwa masikio yako?

Ezekieli 24:27

Siku hiyo kinywa chako kitafumbuliwa kwake aliyeokoka, nawe utasema; hutakuwa bubu tena; ndivyo utakavyokuwa ishara kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.