Ezekieli Mlango 4 Ezekiel

Ezekieli 4:1

Wewe nawe, mwanadamu, jipatie tofali uliweke mbele yako, kisha, chora juu yake mfano wa mji, yaani, Yerusalemu;

Ezekieli 4:2

ukauhusuru, ukajenge ngome juu yake, na kufanya boma juu yake; ukaweke makambi juu yake, na kuweka magogo ya kuubomoa yauzunguke pande zote.

Ezekieli 4:3

Kisha ukajipatie bamba la chuma, ukalisimamishe liwe ukuta wa chuma kati ya wewe na mji huo; ukaelekeze uso wako juu yake, nao utahusuriwa, nawe utauhusuru. Hili litakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.

Ezekieli 4:4

Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao.

Ezekieli 4:5

Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli.

Ezekieli 4:6

Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia.

Ezekieli 4:7

Nawe utauelekeza uso wako, uelekee mazingiwa ya Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake.

Ezekieli 4:8

Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za mazingiwa yako.

Ezekieli 4:9

Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula.

Ezekieli 4:10

Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake.

Ezekieli 4:11

Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake.

Ezekieli 4:12

Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu.

Ezekieli 4:13

Bwana akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza.

Ezekieli 4:14

Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na hayawani; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu.

Ezekieli 4:15

Ndipo akaniambia, Tazama, nimekupa mashonde ya ng'ombe badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo.

Ezekieli 4:16

Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa kushangaa;

Ezekieli 4:17

wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao.