Ezekieli Mlango 14 Ezekiel

Ezekieli 14:1

Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu.

Ezekieli 14:2

Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 14:3

Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?

Ezekieli 14:4

Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake;

Ezekieli 14:5

ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao.

Ezekieli 14:6

Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote.

Ezekieli 14:7

Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, Bwana, nitamjibu, mimi mwenyewe;

Ezekieli 14:8

nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 14:9

Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, Bwana, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.

Ezekieli 14:10

Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno;

Ezekieli 14:11

ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 14:12

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 14:13

Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;

Ezekieli 14:14

wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 14:15

Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao;

Ezekieli 14:16

wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa.

Ezekieli 14:17

Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama;

Ezekieli 14:18

wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; bali wao wenyewe tu wataokoka.

Ezekieli 14:19

Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;

Ezekieli 14:20

wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao.

Ezekieli 14:21

Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama?

Ezekieli 14:22

Lakini, tazama, watasalia mabaki watakaochukuliwa nje, wana na binti; tazama, watawatokea ninyi, nanyi mtaiona njia yao na matendo yao; nanyi mtafarijika katika habari ya mabaya niliyoleta juu ya Yerusalemu, naam, katika habari ya mambo yote niliyoleta juu yake.

Ezekieli 14:23

Nao watawafariji ninyi, mtakapoona njia yao na matendo yao; nanyi mtajua ya kuwa sikufanya bila sababu mambo yote niliyoutenda, asema Bwana MUNGU.