Ezekieli Mlango 22 Ezekiel

Ezekieli 22:1

Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

Ezekieli 22:2

Na wewe, mwanadamu, je! Utauhukumu, utauhukumu mji huu wa damu? Basi uujulishe machukizo yake yote.

Ezekieli 22:3

Nawe utasema, Bwana MUNGU asema hivi; Mji umwagao damu ndani yake, ili wakati wake upate kuja; mji ufanyao vinyago juu ya nafsi yake, ili ujitie unajisi!

Ezekieli 22:4

Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote.

Ezekieli 22:5

Zilizo karibu, na zilizo mbali nawe, zitakudhihaki, Ewe mchafu, uliyejaa fujo.

Ezekieli 22:6

Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu.

Ezekieli 22:7

Ndani yako wamedharau baba na mama; kati yako wamewatenda wageni udhalimu; ndani yako wamewaonea yatima na mjane.

Ezekieli 22:8

Umevidharau vitu vyangu vitakatifu, umezitia unajisi sabato zangu.

Ezekieli 22:9

Wasingiziaji wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu; na ndani yako wamekula juu ya milima; kati yako wamefanya uasherati.

Ezekieli 22:10

Ndani yako wamefunua uchi wa baba zao; ndani yako wamemfanyia nguvu mwanamke asiye safi wakati wa kutengwa kwake.

Ezekieli 22:11

Na mtu mmoja amefanya chukizo pamoja na mke wa jirani yake; na mtu mwingine amemharibu mke wa mwanawe kwa uasherati; na mtu mwingine ndani yako amemfanyia nguvu umbu lake, binti ya babaye.

Ezekieli 22:12

Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 22:13

Basi, tazama, nimeipigia kofi hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo haki, na hiyo damu yako iliyokuwa kati yako.

Ezekieli 22:14

Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, Bwana, nimenena neno hili, tena nitalitenda.

Ezekieli 22:15

Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke.

Ezekieli 22:16

Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 22:17

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 22:18

Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa taka za fedha kwangu; wote wamekuwa shaba, na bati, na chuma, na risasi, kati ya tanuu; wamekuwa taka za fedha.

Ezekieli 22:19

Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi nyote mmekuwa taka za fedha, tazama, nitawakusanya kati ya Yerusalemu.

Ezekieli 22:20

Kama vile watu wakusanyavyo fedha, na shaba, na chuma, na risasi, na bati, kati ya tanuu, ili kuvifukutia moto na kuviyeyusha; ndivyo nitakavyowakusanya ninyi katika hasira yangu, na ghadhabu yangu, nami nitawalaza huko, na kuwayeyusha.

Ezekieli 22:21

Naam, nitawakusanya, na kuwafukutia moto wa ghadhabu yangu, nanyi mtayeyushwa kati yake.

Ezekieli 22:22

Kama fedha iyeyushwavyo kati ya tanuu, ndivyo mtakavyoyeyushwa kati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.

Ezekieli 22:23

Neno la Bwana likanijia, kusema,

Ezekieli 22:24

Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu.

Ezekieli 22:25

Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.

Ezekieli 22:26

Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.

Ezekieli 22:27

Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali.

Ezekieli 22:28

Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo Bwana hakusema neno.

Ezekieli 22:29

Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang'anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki.

Ezekieli 22:30

Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.

Ezekieli 22:31

Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.