Ezekieli Mlango 18 Ezekiel

Ezekieli 18:1

Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

Ezekieli 18:2

Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno?

Ezekieli 18:3

Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli.

Ezekieli 18:4

Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.

Ezekieli 18:5

Bali kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki;

Ezekieli 18:6

hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake;

Ezekieli 18:7

wala hakumdhulumu mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang'anya mtu mali yake kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi;

Ezekieli 18:8

ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake;

Ezekieli 18:9

tena ikiwa amezifuata sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 18:10

Walakini akizaa mwana aliye mnyang'anyi, mmwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo;

Ezekieli 18:11

wala hakutenda mojawapo la mambo hayo yampasayo, bali amekula juu ya milima, na kumtia unajisi mke wa jirani yake,

Ezekieli 18:12

na kuwadhulumu maskini na wahitaji, na kuwanyang'anya watu mali yao kwa nguvu, wala hakurudisha rehani, naye ameviinulia macho vinyago, na kufanya machukizo,

Ezekieli 18:13

naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi baada ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake.

Ezekieli 18:14

Na kama yeye huyo akizaa mwana, naye ameona dhambi zote za baba yake alizozitenda, akaogopa, asifanye neno lo lote kama hayo;

Ezekieli 18:15

hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake,

Ezekieli 18:16

wala hakumdhulumu mtu, wala hakutwaa kitu kiwekwe rehani, wala hakumnyang'anya mtu mali yake kwa nguvu, bali amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwafunika nguo walio uchi;

Ezekieli 18:17

tena ikiwa ameuzuia mkono wake asimwonee maskini, wala hakupokea faida na ziada, naye amezifanya hukumu zangu, na kuzifuata sheria zangu; hatakufa huyu kwa sababu ya uovu wa baba yake, hakika ataishi.

Ezekieli 18:18

Kwa habari za yule baba yake, kwa sababu aliwaonea watu kwa ukali mwingi, na kumnyang'anya ndugu yake mali yake kwa nguvu; na kuyatenda yasiyo mema kati ya watu wake, tazama, atakufa katika uovu wake.

Ezekieli 18:19

Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi.

Ezekieli 18:20

Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.

Ezekieli 18:21

Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa.

Ezekieli 18:22

Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi.

Ezekieli 18:23

Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?

Ezekieli 18:24

Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa.

Ezekieli 18:25

Lakini ninyi mwasema, Njia ya Bwana si sawa. Sikilizeni sasa, Enyi nyumba ya Israeli; Je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa?

Ezekieli 18:26

Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa.

Ezekieli 18:27

Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai.

Ezekieli 18:28

Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.

Ezekieli 18:29

Lakini nyumba ya Israeli husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, je! Njia zangu sizo zilizo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa?

Ezekieli 18:30

Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu.

Ezekieli 18:31

Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli?

Ezekieli 18:32

Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.