Mwanzo Mlango 33 Genesis

Mwanzo 33:1 Genesis 33:1

Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao.

Mwanzo 33:2 Genesis 33:2

Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho.

Mwanzo 33:3 Genesis 33:3

Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake.

Mwanzo 33:4 Genesis 33:4

Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia.

Mwanzo 33:5 Genesis 33:5

Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake.

Mwanzo 33:6 Genesis 33:6

Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama.

Mwanzo 33:7 Genesis 33:7

Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama.

Mwanzo 33:8 Genesis 33:8

Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu.

Mwanzo 33:9 Genesis 33:9

Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako.

Mwanzo 33:10 Genesis 33:10

Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami.

Mwanzo 33:11 Genesis 33:11

Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea.

Mwanzo 33:12 Genesis 33:12

Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia.

Mwanzo 33:13 Genesis 33:13

Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng'ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote.

Mwanzo 33:14 Genesis 33:14

Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri.

Mwanzo 33:15 Genesis 33:15

Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu.

Mwanzo 33:16 Genesis 33:16

Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri.

Mwanzo 33:17 Genesis 33:17

Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi.

Mwanzo 33:18 Genesis 33:18

Yakobo akaja kwa amani mpaka mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji.

Mwanzo 33:19 Genesis 33:19

Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha.

Mwanzo 33:20 Genesis 33:20

Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli.