Mwanzo Mlango 44 Genesis

Mwanzo 44:1 Genesis 44:1

Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake.

Mwanzo 44:2 Genesis 44:2

Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu.

Mwanzo 44:3 Genesis 44:3

Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda zao.

Mwanzo 44:4 Genesis 44:4

Na walipotoka mjini, wala hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema?

Mwanzo 44:5 Genesis 44:5

Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwa hicho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi.

Mwanzo 44:6 Genesis 44:6

Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo.

Mwanzo 44:7 Genesis 44:7

Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya?

Mwanzo 44:8 Genesis 44:8

Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi; tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu, tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa bwana wako fedha au dhahabu?

Mwanzo 44:9 Genesis 44:9

Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu.

Mwanzo 44:10 Genesis 44:10

Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia.

Mwanzo 44:11 Genesis 44:11

Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake.

Mwanzo 44:12 Genesis 44:12

Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini.

Mwanzo 44:13 Genesis 44:13

Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini.

Mwanzo 44:14 Genesis 44:14

Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi.

Mwanzo 44:15 Genesis 44:15

Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi?

Mwanzo 44:16 Genesis 44:16

Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake.

Mwanzo 44:17 Genesis 44:17

Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi enendeni zenu kwa amani kwa baba yenu.

Mwanzo 44:18 Genesis 44:18

Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao.

Mwanzo 44:19 Genesis 44:19

Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu?

Mwanzo 44:20 Genesis 44:20

Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda.

Mwanzo 44:21 Genesis 44:21

Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie.

Mwanzo 44:22 Genesis 44:22

Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa.

Mwanzo 44:23 Genesis 44:23

Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena

Mwanzo 44:24 Genesis 44:24

Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu.

Mwanzo 44:25 Genesis 44:25

Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo.

Mwanzo 44:26 Genesis 44:26

Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi.

Mwanzo 44:27 Genesis 44:27

Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili;

Mwanzo 44:28 Genesis 44:28

mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo.

Mwanzo 44:29 Genesis 44:29

Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini.

Mwanzo 44:30 Genesis 44:30

Basi, nikienda kwa mtumwa wako, baba yangu, na huyu kijana hayupo pamoja nasi, iwapo roho yake imeshikamana na roho ya kijana;

Mwanzo 44:31 Genesis 44:31

itakuwa atakapoona ya kwamba huyu kijana hayuko, atakufa; na watumwa wako watashusha mvi za mtumwa wako, baba yetu, kwa huzuni kaburini.

Mwanzo 44:32 Genesis 44:32

Kwa maana mtumwa wako alijifanya mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, Nisipomrudisha kwako, nitakuwa na hatia kwa baba yangu sikuzote.

Mwanzo 44:33 Genesis 44:33

Basi, sasa nakusihi, uniache mimi mtumwa wako nikae badala ya huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu; na huyu kijana umwache aende pamoja na nduguze.

Mwanzo 44:34 Genesis 44:34

Kwa maana nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami? Nisije nikayaona mabaya yatakayompata baba yangu.