1 Samweli Mlango 22 1st Samuel

1 Samweli 22:1

Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.

1 Samweli 22:2

Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.

1 Samweli 22:3

Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu.

1 Samweli 22:4

Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.

1 Samweli 22:5

Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi.

1 Samweli 22:6

Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka.

1 Samweli 22:7

Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa maakida wa watu elfu, na maakida wa watu mia;

1 Samweli 22:8

hata ninyi nyote mkafanya fitina juu yangu, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemwondokesha mtumishi wangu juu yangu, anivizie kama hivi leo?

1 Samweli 22:9

Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nalimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu.

1 Samweli 22:10

Naye akamwuliza Bwana kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti.

1 Samweli 22:11

Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia.

1 Samweli 22:12

Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu.

1 Samweli 22:13

Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniondokee na kunivizia kama hivi leo?

1 Samweli 22:14

Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako?

1 Samweli 22:15

Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi.

1 Samweli 22:16

Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako.

1 Samweli 22:17

Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa Bwana, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa Bwana.

1 Samweli 22:18

Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, ukawaangukia hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani.

1 Samweli 22:19

Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng'ombe, na punda, na kondoo.

1 Samweli 22:20

Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa jina lake Abiathari, akamkimbilia Daudi.

1 Samweli 22:21

Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa Bwana.

1 Samweli 22:22

Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nalijua yakini ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo.

1 Samweli 22:23

Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.