1 Samweli Mlango 28 1st Samuel

1 Samweli 28:1

Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako.

1 Samweli 28:2

Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinda kichwa changu daima.

1 Samweli 28:3

Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Israeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi.

1 Samweli 28:4

Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa.

1 Samweli 28:5

Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana.

1 Samweli 28:6

Lakini Sauli alipouliza kwa Bwana, Bwana hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii.

1 Samweli 28:7

Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori.

1 Samweli 28:8

Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako.

1 Samweli 28:9

Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?

1 Samweli 28:10

Naye Sauli akamwapia kwa Bwana, akasema, Aishivyo Bwana, haitakupata adhabu yo yote kwa jambo hili.

1 Samweli 28:11

Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli.

1 Samweli 28:12

Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli.

1 Samweli 28:13

Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi.

1 Samweli 28:14

Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia.

1 Samweli 28:15

Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje.

1 Samweli 28:16

Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, akiwa Bwana amekuacha, naye amekuwa adui yako?

1 Samweli 28:17

Yeye Bwana amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; Bwana amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi.

1 Samweli 28:18

Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya Bwana, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii Bwana amekutendea hili leo.

1 Samweli 28:19

Tena pamoja na wewe Bwana atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena Bwana atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti.

1 Samweli 28:20

Mara Sauli akaanguka chini kifulifuli, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yo yote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.

1 Samweli 28:21

Ndipo yule mwanamke akamwendea Sauli, akamwona ya kuwa yeye ametaabika sana, akamwambia, Angalia, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako, nami nimeutia uhai wangu mkononi mwangu, nami nimeyasikiliza maneno yako uliyoniambia.

1 Samweli 28:22

Basi sasa, tafadhali, wewe uisikilize sauti ya mjakazi wako, nikakuandalie ngaa mkate kidogo; ukale, ili upate nguvu, utakapokwenda zako.

1 Samweli 28:23

Lakini yeye alikataa, akasema, Mimi sitaki kula. Ila watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha; naye akaisikiliza sauti yao. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.

1 Samweli 28:24

Naye yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona nyumbani; akafanya haraka kumchinja; akatwaa na unga, akaukanda, akafanya mkate wa mofa kwa unga huo;

1 Samweli 28:25

kisha akamwandalia Sauli na watumishi wake; wakala. Ndipo wakaondoka, wakaenda zao usiku ule.