1 Samweli Mlango 3 1st Samuel

1 Samweli 3:1

Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.

1 Samweli 3:2

Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),

1 Samweli 3:3

na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;

1 Samweli 3:4

basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.

1 Samweli 3:5

Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.

1 Samweli 3:6

Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.

1 Samweli 3:7

Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

1 Samweli 3:8

Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.

1 Samweli 3:9

Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.

1 Samweli 3:10

Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.

1 Samweli 3:11

Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.

1 Samweli 3:12

Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.

1 Samweli 3:13

Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.

1 Samweli 3:14

Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.

1 Samweli 3:15

Naye Samweli akalala hata asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya Bwana. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo.

1 Samweli 3:16

Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa.

1 Samweli 3:17

Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lo lote katika hayo yote Bwana aliyosema nawe.

1 Samweli 3:18

Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lo lote. Naye akasema, Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema.

1 Samweli 3:19

Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.

1 Samweli 3:20

Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana.

1 Samweli 3:21

Naye Bwana akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa Bwana akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la Bwana. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.