1 Samweli Mlango 27 1st Samuel

1 Samweli 27:1

Ndipo Daudi aliposema moyoni mwake, Siku moja, basi, mimi nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jema zaidi kwangu kuliko kukimbia mpaka nchi ya Wafilisti; naye Sauli atakata tamaa kwa habari yangu, asinitafute tena mipakani mwote mwa Israeli; hivyo nitaokoka katika mikono yake.

1 Samweli 27:2

Basi Daudi akaondoka, yeye na hao watu mia sita aliokuwa nao, akamvukia Akishi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.

1 Samweli 27:3

Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali.

1 Samweli 27:4

Naye Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia mpaka Gathi; wala hakumtafuta tena.

1 Samweli 27:5

Daudi akamwambia Akishi, Sasa kama nimeona kibali machoni pako na nipewe mahali katika miji hii mmojawapo mashambani, nipate kukaa huko; mbona mtumwa wako akae katika mji wa kifalme pamoja na wewe?

1 Samweli 27:6

Ndipo Akishi akampa Siklagi siku ile; kwa sababu hiyo huo mji wa Siklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hata hivi leo.

1 Samweli 27:7

Na hesabu ya siku alizokaa Daudi katika nchi ya Wafilisti ilikuwa mwaka mzima na miezi minne.

1 Samweli 27:8

Naye Daudi na watu wake walikuwa wakikwea na kuwashambulia Wageshuri, na Wagirizi, na Waamaleki waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo, tangu Telemu, hapo uendapo Shuri, hata mpaka nchi ya Misri.

1 Samweli 27:9

Tena Daudi akaipiga nchi hiyo, asimhifadhi hai mume wala mke, akateka nyara kondoo, na ng'ombe, na punda, na ngamia na mavazi; kisha akarejea na kufika kwa Akishi.

1 Samweli 27:10

Naye Akishi humwuliza, Je! Mmeshambulia upande gani leo? Na Daudi husema, Juu ya Negebu ya Yuda, au, juu ya Negebu ya Wayerameeli, au, juu ya Negebu ya Wakeni.

1 Samweli 27:11

Tena Daudi hakumhifadhi hai mume wala mke, ili kuwaleta Gathi maana alisema, Wasituchongee kusema, Ndivyo alivyofanya Daudi, tena ndivyo ilivyokuwa desturi yake wakati wote alipokaa katika nchi ya Wafilisti.

1 Samweli 27:12

Hivyo Akishi akamsadiki Daudi, akasema, Amewachukiza kabisa hao watu wake Israeli; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu hata milele.