1 Samweli Mlango 15 1st Samuel

1 Samweli 15:1

Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, Bwana alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya Bwana.

1 Samweli 15:2

Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.

1 Samweli 15:3

Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.

1 Samweli 15:4

Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.

1 Samweli 15:5

Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.

1 Samweli 15:6

Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.

1 Samweli 15:7

Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.

1 Samweli 15:8

Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.

1 Samweli 15:9

Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng'ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa.

1 Samweli 15:10

Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema,

1 Samweli 15:11

Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha.

1 Samweli 15:12

Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.

1 Samweli 15:13

Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na Bwana, nimeitimiza amri ya Bwana.

1 Samweli 15:14

Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng'ombe ninaousikia?

1 Samweli 15:15

Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.

1 Samweli 15:16

Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.

1 Samweli 15:17

Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.

1 Samweli 15:18

Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.

1 Samweli 15:19

Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?

1 Samweli 15:20

Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.

1 Samweli 15:21

Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.

1 Samweli 15:22

Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.

1 Samweli 15:23

Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.

1 Samweli 15:24

Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.

1 Samweli 15:25

Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.

1 Samweli 15:26

Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.

1 Samweli 15:27

Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.

1 Samweli 15:28

Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.

1 Samweli 15:29

Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.

1 Samweli 15:30

Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu Bwana, Mungu wako.

1 Samweli 15:31

Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu Bwana.

1 Samweli 15:32

Ndipo Samweli akasema, Nileteeni hapa Agagi, mfalme wa Waamaleki. Basi Agagi akamwendea kwa utepetevu. Naye Agagi akasema, Bila shaka uchungu wa mauti umeondoka.

1 Samweli 15:33

Lakini Samweli akamjibu, Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, vivyo hivyo mama yako atafiwa miongoni mwa wanawake. Basi Samweli akamkata Agagi vipande mbele za Bwana huko Gilgali.

1 Samweli 15:34

Na baada ya hayo Samweli akaenda zake kule Rama; naye Sauli akakwea kwenda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli.

1 Samweli 15:35

Wala Samweli hakuenda tena kuonana na Sauli hata siku ya kufa kwake; lakini Samweli alikuwa akimlilia Sauli; naye Bwana akaghairi ya kuwa amemtawaza Sauli awe mfalme juu ya Israeli.