1 Samweli Mlango 10 1st Samuel

1 Samweli 10:1

Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake.

1 Samweli 10:2

Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu?

1 Samweli 10:3

Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai;

1 Samweli 10:4

nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao.

1 Samweli 10:5

Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri;

1 Samweli 10:6

na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.

1 Samweli 10:7

Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.

1 Samweli 10:8

Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya.

1 Samweli 10:9

Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile.

1 Samweli 10:10

Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao.

1 Samweli 10:11

Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

1 Samweli 10:12

Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n'nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

1 Samweli 10:13

Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu.

1 Samweli 10:14

Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli.

1 Samweli 10:15

Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje?

1 Samweli 10:16

Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo.

1 Samweli 10:17

Basi Samweli akawakusanya watu mbele za Bwana huko Mispa

1 Samweli 10:18

akawaambia wana wa Israeli, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea;

1 Samweli 10:19

lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za Bwana, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu.

1 Samweli 10:20

Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa.

1 Samweli 10:21

Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana.

1 Samweli 10:22

Basi wakazidi kumwuliza Bwana, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye Bwana akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo.

1 Samweli 10:23

Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu.

1 Samweli 10:24

Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na Bwana, ya kuwa hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi!

1 Samweli 10:25

Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za Bwana. Samweli akawaruhusu watu wote, waende kila mtu nyumbani kwake.

1 Samweli 10:26

Sauli naye akaenda nyumbani kwake huko Gibea; na pamoja naye wakaenda kikosi cha watu, ambao Mungu alikuwa ameigusa mioyo yao.

1 Samweli 10:27

Walakini wengine wasiofaa kitu wakasema, Huyu je! Atatuokoaje? Nao wakamdharau, wasimletee zawadi.