1 Samweli Mlango 31 1st Samuel

1 Samweli 31:1

Basi Wafilisti wakapigana na Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima wa Gilboa.

1 Samweli 31:2

Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli.

1 Samweli 31:3

Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde.

1 Samweli 31:4

Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao; wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanichoma, na kunisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.

1 Samweli 31:5

Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa pamoja naye.

1 Samweli 31:6

Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu, na mchukua silaha zake, na watu wake wote pamoja siku iyo hiyo.

1 Samweli 31:7

Kisha watu wa Israeli waliokuwa upande wa pili wa bonde lile, na ng'ambo ya Yordani, walipoona ya kuwa watu wa Israeli wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo.

1 Samweli 31:8

Hata ikawa, siku ya pili yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara waliouawa, walimwona Sauli na wanawe watatu wameanguka juu ya mlima wa Gilboa.

1 Samweli 31:9

Wakamkata kichwa, wakamvua silaha zake, wakapeleka wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari nyumbani mwa sanamu zao, na kwa watu.

1 Samweli 31:10

Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa Maashtorethi; wakakitundika kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-shani.

1 Samweli 31:11

Na wenyeji wa Yabesh-Gileadi waliposikia habari zake, jinsi hao Wafilisti walivyomtenda Sauli,

1 Samweli 31:12

wakainuka mashujaa wote, wakaenda usiku kucha, wakautwaa mwili wake Sauli, na miili ya wanawe, na kuiondoa ukutani kwa Beth-shani nao wakaja Yabeshi, na kuiteketeza huko.

1 Samweli 31:13

Kisha wakaitwaa mifupa yao, na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.