1 Samweli Mlango 8 1st Samuel

1 Samweli 8:1

Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli.

1 Samweli 8:2

Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba.

1 Samweli 8:3

Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu.

1 Samweli 8:4

Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;

1 Samweli 8:5

wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.

1 Samweli 8:6

Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.

1 Samweli 8:7

Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.

1 Samweli 8:8

Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.

1 Samweli 8:9

Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.

1 Samweli 8:10

Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana.

1 Samweli 8:11

Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.

1 Samweli 8:12

Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.

1 Samweli 8:13

Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.

1 Samweli 8:14

Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.

1 Samweli 8:15

Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.

1 Samweli 8:16

Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe.

1 Samweli 8:17

Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.

1 Samweli 8:18

Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; Bwana asiwajibu siku ile.

1 Samweli 8:19

Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu;

1 Samweli 8:20

ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu.

1 Samweli 8:21

Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana.

1 Samweli 8:22

Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake.