1 Samweli Mlango 21 1st Samuel

1 Samweli 21:1

Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwani wewe kuwa peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe?

1 Samweli 21:2

Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani.

1 Samweli 21:3

Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au cho chote ulicho nacho hapa.

1 Samweli 21:4

Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya sikuzote chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake.

1 Samweli 21:5

Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi?

1 Samweli 21:6

Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za Bwana, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa.

1 Samweli 21:7

Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za Bwana jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli.

1 Samweli 21:8

Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka.

1 Samweli 21:9

Yule kuhani akasema, upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe.

1 Samweli 21:10

Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi.

1 Samweli 21:11

Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake.

1 Samweli 21:12

Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi.

1 Samweli 21:13

Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake.

1 Samweli 21:14

Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu?

1 Samweli 21:15

Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?