2 Mambo ya Nyakati Mlango 18 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 18:1

Basi, Yehoshafati alikuwa na mali na heshima tele, tena akafanya ujamaa na Ahabu.

2 Mambo ya Nyakati 18:2

Hata baada ya miaka kadha wa kadha akamshukia Ahabu huko Samaria. Ahabu akamchinjia kondoo na ng'ombe tele, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, akamshawishi ili apande pamoja naye waende Ramoth-gileadi.

2 Mambo ya Nyakati 18:3

Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Je! Utakwenda nami mpaka Ramoth-gileadi? Akamjibu, Mimi ni kama wewe, na watu wangu kama watu wako; nasi tutakuwa pamoja nawe vitani.

2 Mambo ya Nyakati 18:4

Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 18:5

Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii, watu mia nne; akawaambia, Je! Tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Wakasema, Kwea; kwa kuwa Mungu atautia mkononi mwa mfalme.

2 Mambo ya Nyakati 18:6

Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye?

2 Mambo ya Nyakati 18:7

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema kamwe, ila siku zote mabaya; naye ndiye Mikaya mwana wa Imla. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi.

2 Mambo ya Nyakati 18:8

Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla.

2 Mambo ya Nyakati 18:9

Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye sakafu pa kuingilia lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao.

2 Mambo ya Nyakati 18:10

Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia.

2 Mambo ya Nyakati 18:11

Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.

2 Mambo ya Nyakati 18:12

Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema.

2 Mambo ya Nyakati 18:13

Mikaya akasema, Kama aishivyo Bwana, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena.

2 Mambo ya Nyakati 18:14

Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu.

2 Mambo ya Nyakati 18:15

Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?

2 Mambo ya Nyakati 18:16

Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.

2 Mambo ya Nyakati 18:17

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

2 Mambo ya Nyakati 18:18

Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.

2 Mambo ya Nyakati 18:19

Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

2 Mambo ya Nyakati 18:20

Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani?

2 Mambo ya Nyakati 18:21

Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo.

2 Mambo ya Nyakati 18:22

Basi sasa, angalia, Bwana ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye Bwana amenena mabaya juu yako.

2 Mambo ya Nyakati 18:23

Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu roho ya Bwana ili aseme na wewe?

2 Mambo ya Nyakati 18:24

Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.

2 Mambo ya Nyakati 18:25

Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme;

2 Mambo ya Nyakati 18:26

mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.

2 Mambo ya Nyakati 18:27

Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

2 Mambo ya Nyakati 18:28

Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-gileadi.

2 Mambo ya Nyakati 18:29

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha; nao wakaingia vitani.

2 Mambo ya Nyakati 18:30

Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru maakida wa magari yake, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.

2 Mambo ya Nyakati 18:31

Ikawa maakida wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Mfalme wa Israeli ni huyu. Basi wakamgeukia ili wapigane naye; lakini Yehoshafati akalia, na Bwana akamsaidia; Mungu akawafarakisha kwake.

2 Mambo ya Nyakati 18:32

Ikawa, maakida wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.

2 Mambo ya Nyakati 18:33

Na mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.

2 Mambo ya Nyakati 18:34

Pigano likazidi siku ile; lakini mfalme wa Israeli akajitegemeza garini juu ya Washami hata jioni; akafa kama wakati wa kuchwa kwa jua.