2 Mambo ya Nyakati Mlango 20 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 20:1

Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani.

2 Mambo ya Nyakati 20:2

Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi).

2 Mambo ya Nyakati 20:3

Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute Bwana; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote.

2 Mambo ya Nyakati 20:4

Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute Bwana; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 20:5

Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa Bwana, mbele ya ua mpya;

2 Mambo ya Nyakati 20:6

akasema, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako.

2 Mambo ya Nyakati 20:7

Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele?

2 Mambo ya Nyakati 20:8

Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema,

2 Mambo ya Nyakati 20:9

Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa.

2 Mambo ya Nyakati 20:10

Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu;

2 Mambo ya Nyakati 20:11

tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha.

2 Mambo ya Nyakati 20:12

Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako.

2 Mambo ya Nyakati 20:13

Wakasimama Yuda wote mbele za Bwana, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao.

2 Mambo ya Nyakati 20:14

Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya Bwana, katikati ya kusanyiko;

2 Mambo ya Nyakati 20:15

akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.

2 Mambo ya Nyakati 20:16

Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli.

2 Mambo ya Nyakati 20:17

Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa Bwana ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa Bwana yu pamoja nanyi.

2 Mambo ya Nyakati 20:18

Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 20:19

Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.

2 Mambo ya Nyakati 20:20

Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.

2 Mambo ya Nyakati 20:21

Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia Bwana, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni Bwana; kwa maana fadhili zake ni za milele.

2 Mambo ya Nyakati 20:22

Nao walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa.

2 Mambo ya Nyakati 20:23

Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe.

2 Mambo ya Nyakati 20:24

Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka.

2 Mambo ya Nyakati 20:25

Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana.

2 Mambo ya Nyakati 20:26

Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia Bwana; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo.

2 Mambo ya Nyakati 20:27

Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa Bwana amewafurahisha juu ya adui zao.

2 Mambo ya Nyakati 20:28

Wakafika Yerusalemu wenye vinanda vinubi na mapanda kwenda nyumbani kwa Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 20:29

Ikawa hofu ya Mungu juu ya falme zote za nchi, waliposikia ya kuwa Bwana amepigana juu ya adui za Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 20:30

Basi ukatulia ufalme wake Yehoshafati; kwa sababu Mungu wake alimstarehesha pande zote.

2 Mambo ya Nyakati 20:31

Yehoshafati akatawala juu ya Yuda; alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi.

2 Mambo ya Nyakati 20:32

Akaiendea njia ya Asa babaye, wala hakuiacha, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 20:33

Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; wala mioyo ya watu bado haijakazwa kwa Mungu wa baba zao.

2 Mambo ya Nyakati 20:34

Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, angalia, yameandikwa katika tarehe ya Yehu mwana wa Hanani, iliyotiwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 20:35

Baada ya hayo Yehoshafati mfalme wa Yuda akapatana na Ahazia mfalme wa Israeli; naye huyo ndiye aliyefanya mabaya mno;

2 Mambo ya Nyakati 20:36

akapatana naye kufanya merikebu za kuendea Tarshishi; wakazifanya merikebu zile huko Esion-geberi.

2 Mambo ya Nyakati 20:37

Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii juu ya Yehoshafati, akasema, Kwa sababu umepatana na Ahazia, Bwana amezivunja-vunja kazi zako. Zikavunjika merikebu, zisiweze kufika Tarshishi.