2 Mambo ya Nyakati Mlango 4 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 4:1

Tena akafanya madhabahu ya shaba, mikono ishirini urefu wake, na mikono ishirini upana wake, na mikono kumi kwenda juu kwake.

2 Mambo ya Nyakati 4:2

Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ya mviringo, na kwenda juu kwake ilikuwa mikono mitano; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.

2 Mambo ya Nyakati 4:3

Na chini yake palikuwa na mifano ya ng'ombe, walioizunguka pande zote ,kwa mikono kumi,wakiizunguka pande zote ile bahari. Ng`ombe walikuwa safu mbili ,wakayeyushwa hapo ilipoyeyushwa hiyo bahari.

2 Mambo ya Nyakati 4:4

Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.

2 Mambo ya Nyakati 4:5

Na unene wake ulikuwa nyanda nne, na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu tatu, kukaa ndani yake.

2 Mambo ya Nyakati 4:6

Akafanya na birika kumi, akaziweka tano upande wa kuume, na tano upande wa kushoto, za kuoshea; ndizo walizooshea mambo ya kafara; lakini hiyo bahari ilikuwa ya makuhani ya kuogea.

2 Mambo ya Nyakati 4:7

Akavifanya vinara vya taa kumi vya dhahabu, kadiri ya vilivyoagiziwa; akavitia hekaluni, vitano upande wa kuume, na vitano upande wa kushoto.

2 Mambo ya Nyakati 4:8

Akafanya na meza kumi, akazitia hekaluni, tano upande wa kuume, na tano upande wa kushoto. Kisha akafanya mabakuli mia ya dhahabu.

2 Mambo ya Nyakati 4:9

Tena akaufanya ua wa makuhani, na ua mkubwa, nayo milango yake, akaifunikiza kwa shaba milango yake.

2 Mambo ya Nyakati 4:10

Nayo bahari akaiweka upande wa kuume kwa mashariki, kuelekea kusini.

2 Mambo ya Nyakati 4:11

Na Huramu akayafanya masufuria, na majembe, na mabakuli. Basi Huramu akamaliza kufanya hiyo kazi, aliyomfanyia mfalme Sulemani ya nyumba ya Mungu;

2 Mambo ya Nyakati 4:12

zile nguzo mbili, na vimbe, na taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo; nazo nyavu mbili za kuzifunika vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo;

2 Mambo ya Nyakati 4:13

na makomamanga mia nne ya nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuzifunika vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo.

2 Mambo ya Nyakati 4:14

Akayafanya na matako, na mabirika akafanya juu ya matako;

2 Mambo ya Nyakati 4:15

bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini yake.

2 Mambo ya Nyakati 4:16

Masufuria pia, na majembe, na nyuma, na vyombo vyake vyote, Huramu akamfanyia mfalme Sulemani kwa nyumba ya BWANA ,vya shaba iliyokatuka.

2 Mambo ya Nyakati 4:17

Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sereda.

2 Mambo ya Nyakati 4:18

Ndivyo alivyovifanya Sulemani vyombo hivyo vyote, vingi sana; kwa kuwa uzani wa shaba ulikuwa hautafutikani.

2 Mambo ya Nyakati 4:19

Basi Sulemani akavifanya vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa Mungu, madhabahu ya dhahabu pia, nazo meza, ambazo juu yake iliwekwa mikate ya wonyesho;

2 Mambo ya Nyakati 4:20

na vinara na taa zake, ziwake kama ilivyoagizwa mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu iliyosafika;

2 Mambo ya Nyakati 4:21

na maua, na taa, na makoleo, ya dhahabu, ndiyo dhahabu bora;

2 Mambo ya Nyakati 4:22

na mikasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu iliyosafika; na kwa habari za mahali pa kuingia nyumbani, milango yake ya ndani ya patakatifu pa patakatifu, na milango ya nyumba, yaani ya hekalu, ilikuwa ya dhahabu.