2 Mambo ya Nyakati Mlango 32 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 32:1

:Ikawa, baada ya mambo hayo, na uaminifu huo, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akaja, akaingia katika Yuda, akafanya marago juu ya miji yenye maboma, akadhania kwamba ataipata iwe yake.

2 Mambo ya Nyakati 32:2

Basi Hezekia, alipoona ya kuwa Senakeribu amekuja, na kuazimia kupigana na Yerusalemu,

2 Mambo ya Nyakati 32:3

akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia.

2 Mambo ya Nyakati 32:4

Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?

2 Mambo ya Nyakati 32:5

Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.

2 Mambo ya Nyakati 32:6

Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,

2 Mambo ya Nyakati 32:7

Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;

2 Mambo ya Nyakati 32:8

kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo Bwana, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.

2 Mambo ya Nyakati 32:9

Na baada ya hayo Senakeribu mfalme wa Ashuru, akatuma watumishi wake waende Yerusalemu, (naye alikuwapo mbele ya Lakishi, na uwezo wake wote pamoja naye,) kwa Hezekia, mfalme wa Yuda, na kwa Yuda wote waliokuwako Yerusalemu, kusema,

2 Mambo ya Nyakati 32:10

Senakeribu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Mwatumainia nini hata mkae mkihusuriwa katika Yerusalemu?

2 Mambo ya Nyakati 32:11

Siye Hezekia anayewashawishi, mtolewe kufa kwa njaa na kwa kiu, akisema, Bwana, Mungu wetu, atatuokoa na mkono wa mfalme wa Ashuru?

2 Mambo ya Nyakati 32:12

Si yeye Hezekia huyo aliyeondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaamuru Yuda na Yerusalemu, akisema, Abuduni mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtafukiza uvumba?

2 Mambo ya Nyakati 32:13

Je! Ninyi hamjui mimi na baba zangu tuliyowafanyia watu wote wa nchi? Je! Miungu ya mataifa wa nchi iliweza kuokoa kwa lo lote nchi zao na mkono wangu?

2 Mambo ya Nyakati 32:14

Ni yupi miongoni mwa miungu ya mataifa wale walioharibiwa kabisa na baba zangu, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, hata Mungu wenu aweze kuwaokoa ninyi na mkono wangu?

2 Mambo ya Nyakati 32:15

Basi sasa asiwadanganye Hezekia, wala asiwashawishi kwa hayo, wala msimwamini; kwa kuwa hapana mungu wa taifa lo lote, wala wa ufalme wo wote, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, au na mkono wa baba zangu; sembuse Mungu wenu atawaokoaje ninyi na mkono wangu?

2 Mambo ya Nyakati 32:16

Na watumishi wake wakazidi kusema juu ya Bwana Mungu, na juu ya Hezekia, mtumishi wake.

2 Mambo ya Nyakati 32:17

Tena akaandika waraka, kumtukana Bwana, Mungu wa Israeli, na kumwambia, akisema, Kama vile miungu ya mataifa wa nchi isivyowaokoa watu wao na mkono wangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hatawaokoa watu wake na mkono wangu.

2 Mambo ya Nyakati 32:18

Wakawalilia kwa sauti kuu, kwa lugha ya Kiyahudi, watu wa Yerusalemu waliokuwako ukutani ili kuwaogofisha, na kuwafadhaisha; hata wapate kuutwaa mji.

2 Mambo ya Nyakati 32:19

Wakamnenea Mungu wa Yerusalemu, kana kwamba kuitaja miungu ya mataifa wa nchi, iliyo kazi ya mikono ya watu.

2 Mambo ya Nyakati 32:20

Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.

2 Mambo ya Nyakati 32:21

Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.

2 Mambo ya Nyakati 32:22

Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.

2 Mambo ya Nyakati 32:23

Watu wengi walimletea Bwana zawadi huko Yerusalemu, na vitu vya thamani kwa Hezekia, mfalme wa Yuda; hata yeye akatukuka tangu wakati ule machoni pa mataifa yote.

2 Mambo ya Nyakati 32:24

Katika siku hizo Hezekia akaugua akawa katika hatari ya kufa; akamwomba Bwana; naye akasema naye, akampa ishara.

2 Mambo ya Nyakati 32:25

Walakini kadiri alivyofadhiliwa Hezekia hakumrudishia vivyo; kwa kuwa moyo wake ulitukuka; kwa hiyo ikawako hasira juu yake, na juu ya Yuda na Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 32:26

Hata hivyo Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya Bwana siku za Hezekia.

2 Mambo ya Nyakati 32:27

Naye Hezekia akawa na mali nyingi mno na heshima; akajifanyizia hazina za fedha, na za dhahabu, na za vito, na za manukato, na za ngao, na za namna zote za vyombo vya thamani;

2 Mambo ya Nyakati 32:28

ghala pia za mazao ya nafaka na mvinyo na mafuta; na malisho ya wanyama wa namna zote, na makundi mazizini.

2 Mambo ya Nyakati 32:29

Tena akajifanyizia miji, na mali za kondoo na ng'ombe kwa wingi; maana Mungu alimtajirisha sana sana.

2 Mambo ya Nyakati 32:30

Naye huyo Hezekia ndiye aliyezuia chemchemi ya juu ya maji ya Gihoni, akayaleta chini moja kwa moja upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Akafanikiwa Hezekia katika kazi zake zote.

2 Mambo ya Nyakati 32:31

Walakini kwa habari ya wajumbe wa wakuu wa Babeli, waliotuma kwake kuuliza ajabu iliyofanywa katika nchi, Mungu akamwacha, ili amjaribu, ili kwamba ayajue yote yaliyokuwamo moyoni mwake.

2 Mambo ya Nyakati 32:32

Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na matendo yake mema, tazama, yameandikwa katika maono ya Isaya nabii, mwana wa Amozi, katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 32:33

Hezekia akalala na babaze, wakamzika mahali pa kupandia makaburi ya wana wa Daudi; nao Yuda wote na wenyeji wa Yerusalemu wakamfanyia heshima alipokufa. Na Manase mwanawe akatawala mahali pake.