2 Mambo ya Nyakati Mlango 14 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 14:1

Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi.

2 Mambo ya Nyakati 14:2

Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa Bwana, Mungu wake;

2 Mambo ya Nyakati 14:3

maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera;

2 Mambo ya Nyakati 14:4

akawaamuru Yuda wamtafute Bwana, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri.

2 Mambo ya Nyakati 14:5

Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake.

2 Mambo ya Nyakati 14:6

Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu Bwana amemstarehesha.

2 Mambo ya Nyakati 14:7

Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta Bwana, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa.

2 Mambo ya Nyakati 14:8

Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa.

2 Mambo ya Nyakati 14:9

Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha.

2 Mambo ya Nyakati 14:10

Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha.

2 Mambo ya Nyakati 14:11

Naye Asa akamlilia Bwana, Mungu wake, akasema, Bwana, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee Bwana, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu.

2 Mambo ya Nyakati 14:12

Basi, Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia.

2 Mambo ya Nyakati 14:13

Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; nao wengi wakaanguka wa Wakushi hata wasiweze kupona; kwa sababu waliangamizwa mbele za Bwana, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka mengi sana.

2 Mambo ya Nyakati 14:14

Wakaipiga miji yote kando-kando ya Gerari; maana hofu ya Bwana ikawajia; nao wakaiteka nyara miji yote, kwa maana zilikuwamo ndani yake nyara nyingi mno.

2 Mambo ya Nyakati 14:15

Wakazipiga pia hema za ng'ombe, wakachukua kondoo wengi na ngamia, wakarudi Yerusalemu.