2 Mambo ya Nyakati Mlango 24 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 24:1

Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Sibia wa Beer-sheba.

2 Mambo ya Nyakati 24:2

Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana siku zote za Yehoyada kuhani.

2 Mambo ya Nyakati 24:3

Yehoyada akamwoza wake wawili, naye akazaa wana na binti.

2 Mambo ya Nyakati 24:4

Ikawa baada ya haya, Yoashi alikuwa na nia ya kuitengeneza nyumba ya Mungu.

2 Mambo ya Nyakati 24:5

Akawakusanya makuhani na Walawi, akawaambia, Nendeni mijini mwa Yuda, mkakusanye katika Israeli wote fedha, ili kuitengeneza nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka, mkafanye bidii kuliharakisha neno hili. Walakini Walawi hawakuliharakisha.

2 Mambo ya Nyakati 24:6

Mfalme akamwita Yehoyada mkuu wao, akamwambia, Mbona hukuwataka Walawi waitoze Yuda na Yerusalemu kodi ya Musa mtumishi wa Bwana, na ya kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya hema ya ushuhuda?

2 Mambo ya Nyakati 24:7

Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya Bwana wamewapatia mabaali.

2 Mambo ya Nyakati 24:8

Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 24:9

Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea Bwana kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani.

2 Mambo ya Nyakati 24:10

Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha.

2 Mambo ya Nyakati 24:11

Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele.

2 Mambo ya Nyakati 24:12

Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya Bwana; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya Bwana, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 24:13

Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara.

2 Mambo ya Nyakati 24:14

Nao walipokwisha, wakaleta mbele ya mfalme na Yehoyada fedha iliyobaki, vikafanyizwa kwayo vyombo vya nyumba ya Bwana, vyombo vya utumishi, navyo vya kutolea, na miiko, na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Bwana, daima, siku zote za Yehoyada.

2 Mambo ya Nyakati 24:15

Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye umri mwingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia na thelathini.

2 Mambo ya Nyakati 24:16

Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.

2 Mambo ya Nyakati 24:17

Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.

2 Mambo ya Nyakati 24:18

Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.

2 Mambo ya Nyakati 24:19

Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.

2 Mambo ya Nyakati 24:20

Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.

2 Mambo ya Nyakati 24:21

Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 24:22

Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.

2 Mambo ya Nyakati 24:23

Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote.

2 Mambo ya Nyakati 24:24

Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu.

2 Mambo ya Nyakati 24:25

Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.

2 Mambo ya Nyakati 24:26

Na hawa ndio waliomfanyia fitina, Zabadi mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, na Yehozabadi mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabi.

2 Mambo ya Nyakati 24:27

Basi kwa habari ya wanawe, na ukubwa wa mizigo aliolemewa, na majengo ya nyumba ya Mungu, tazama, hayo yameandikwa katika maelezo ya kitabu cha wafalme. Na Amazia mwanawe akatawala mahali pake.