2 Mambo ya Nyakati Mlango 5 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 5:1

Hivyo ikaisha kazi yote Sulemani aliyoifanyia nyumba ya Bwana. Sulemani akaviingiza vitu alivyovitakasa baba yake Daudi; fedha, na dhahabu, na vyombo vyote, akavitia ndani ya hazina za nyumba ya Mungu.

2 Mambo ya Nyakati 5:2

Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni.

2 Mambo ya Nyakati 5:3

Wakakutana watu wote wa Israeli mbele ya mfalme wakati wa sikukuu, katika mwezi wa saba.

2 Mambo ya Nyakati 5:4

Wakaja wazee wote wa Israeli, nao Walawi wakajitwika sanduku.

2 Mambo ya Nyakati 5:5

Wakalipandisha sanduku, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwamo Hemani, vitu hivyo makuhani Walawi wakavipandisha.

2 Mambo ya Nyakati 5:6

Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli, waliokutanika kwake, walikuwako mbele ya sanduku, wakichinja dhabihu za kondoo na ng'ombe, wasiohesabika wala kujumlishwa kwa kuwa wengi.

2 Mambo ya Nyakati 5:7

Makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Bwana mahali pake katika chumba cha ndani cha nyumba, patakatifu pa patakatifu, yaani, chini ya mabawa ya makerubi.

2 Mambo ya Nyakati 5:8

Kwa maana makerubi yalinyosha mabawa yao juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.

2 Mambo ya Nyakati 5:9

Na ile miti ilikuwa mirefu, hata ncha za miti zilionekana sandukuni mbele ya chumba cha ndani, lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo.

2 Mambo ya Nyakati 5:10

Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili alizozitia Musa huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka Misri.

2 Mambo ya Nyakati 5:11

Ikawa makuhani walipokwisha kutoka katika patakatifu; (kwani makuhani wote waliokuwapo, walikuwa wamejitakasa, wala hawakuzishika zamu zao;

2 Mambo ya Nyakati 5:12

tena Walawi waimbaji, wote pia, yaani Asafu, na Hemani, na Yeduthuni, na wana wao, na ndugu zao, hali wamevaa kitani safi, wenye matoazi na vinanda na vinubi, wamesimama upande wa mashariki wa madhabahu, na pamoja nao makuhani mia na ishirini wakipiga panda;)

2 Mambo ya Nyakati 5:13

hata ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja ya kumsifu na kumshukuru Bwana nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na vinanda, wakimsifu Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya Bwana,

2 Mambo ya Nyakati 5:14

hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa Bwana.