2 Mambo ya Nyakati Mlango 21 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 21:1

Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; akatawala Yehoramu mwanawe mahali pake.

2 Mambo ya Nyakati 21:2

Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, na Yehieli, na Zekaria, na Azaria, na Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 21:3

Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, na za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza.

2 Mambo ya Nyakati 21:4

Basi Yehoramu alipoinuliwa juu ya ufalme wa babaye, na kujitia nguvu, akawaua nduguze wote kwa upanga, na baadhi ya wakuu wa Israeli pia.

2 Mambo ya Nyakati 21:5

Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 21:6

Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya maovu machoni pa Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 21:7

Walakini Bwana hakupenda kuiharibu nyumba ya Daudi, kwa sababu ya agano alilolifanya na Daudi, na kama alivyomwahidi kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote.

2 Mambo ya Nyakati 21:8

Zamani zake Edomu wakaasi chini ya mkono wa Yuda, wakajifanyia mfalme.

2 Mambo ya Nyakati 21:9

Ndipo akavuka Yehoramu na maakida wake, na magari yake yote pamoja naye; akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na hao maakida wa magari.

2 Mambo ya Nyakati 21:10

Hivyo Edomu wakaasi chini ya mkono wa Yuda, hata leo; wakaasi na Libna zamani zizo hizo chini ya mkono wake: kwa sababu alikuwa amemwacha Bwana, Mungu wa baba zake.

2 Mambo ya Nyakati 21:11

Tena ndiye aliyefanya mahali pa juu milimani pa Yuda, na kuwaendesha katika uasherati wenyeji wa Yerusalemu, na kuwakosesha Yuda.

2 Mambo ya Nyakati 21:12

Likamjia andiko kutoka kwa Eliya nabii, kusema, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa sababu hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda;

2 Mambo ya Nyakati 21:13

lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, ukawaendesha katika uasherati Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe;

2 Mambo ya Nyakati 21:14

tazama, Bwana atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote;

2 Mambo ya Nyakati 21:15

nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku.

2 Mambo ya Nyakati 21:16

Bwana akawaamsha roho Wafilisti, na Waarabu waliowaelekea Wakushi juu ya Yehoramu,

2 Mambo ya Nyakati 21:17

nao wakakwea juu ya nchi ya Yuda, wakaipenya, wakaichukua mali yote iliyoonekama nyumbani mwa mfalme, na wanawe pia, na wakeze; asisaziwe mwana hata mmoja, ila Ahazia, aliyekuwa mdogo miongoni mwa wanawe.

2 Mambo ya Nyakati 21:18

Na baada ya hayo yote Bwana akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka.

2 Mambo ya Nyakati 21:19

Ikawa baada ya siku, ikiisha miaka miwili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiugua vibaya. Wala watu wake hawakumfukizia mafukizo kama ya baba zake.

2 Mambo ya Nyakati 21:20

Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu miaka minane; akafariki bila kutamaniwa; wakamzika mjini mwa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme.